Pigo jingine kwa Aukot bunge la kaunti ya Lamu kuupiga teke mswada wa Punguza Mizigo
Na KALUME KAZUNGU
KIONGOZI wa Thirdway Alliance, Bw Ekuru Aukot, amepata pigo jingine baada ya Bunge la Kaunti ya Lamu kujiunga na mengine kadha ambayo yameangusha mswada wa Punguza Mizigo.
Mswada huo ulikuwa umewasilishwa bungeni na Mwakilishi wa Wadi ya Hongwe, Bw James Komu lakini akakosa wa kumuunga mkono, hivyo mswada huo kutupiliwa mbali moja kwa moja.
Hali sawia na hiyo ilifanyika kwenye mabunge ya Kaunti za Kirinyaga na Nyamira, ambapo mswada wa Punguza Mizigo ulipigwa teke baada ya kukosa mtu wa kwanza wa kuunga mkono mswada huo.
Kulingana na Sheria za Bunge, mswada wowote ukikosa mtu wa kwanza wa kuunga mkono, hulazimika kusitishwa kwa kipindi cha miezi sita kwanza, ambapo baadaye unaweza kuwasilishwa kwa mara nyingine bungeni ili kujadiliwa na ama kupitishwa au kuangushwa.
Aidha kulingana na muda mfupi uliosalia wa mswada huo kuwasilishwa, ni dhahiri kwamba Bunge la Kaunti ya Lamu limeukataa mswada huo.
Akizungumza muda mfupi baada ya Bunge la Lamu kuupiga teke mswada huo, Bw Komu – katika kuonekana kukiri na hata kwa kinaya – alisema mswada huo una udhaifu mwingi, ikizingatiwa kuwa miongoni mwa mapendekezo yake ni kupunguza idadi ya wabunge na pia maeneobunge nchini.
“Ikiwa maeneobunge yatapunguzwa, hiyo inadhihirisha kuwa baadhi ya wadi zetu hapa nchini pia zitafyekwa. Mimi nilichukua jukumu la kuuwasilisha mswada bungeni lakini hakuna aliyeniunga mkono. Kuna uwezekano kwamba mswada ukikosa uungwaji mkono unasitishwa kwanza na kisha kurudishwa bungeni baada ya miezi sita. Lakini kwa sasa ni dhahiri kwamba tumeukataa mswada huo wa Punguza Mizigo hapa Lamu, ikizingatiwa kuwa zimesalia tu siku chache mswada huo upitishwe au uangushwe nchini,” akasema Bw Komu.
Mwakilishi Maalum wa Bunge la Kaunti ya Lamu, Bi Amina Kale aliwapongeza madiwani wenzake kwa kukataa mswada wa Punguza Mizigo.
Bi Kale aliukosoa mswada huo kwa kupendekeza kuondolewa kwa nafasi ya Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti na pia vyeo vya vyote vya wawakilishi maalum.
Jinsia ya kike
Alisema yeye haungi mkono mswada wowote unaopendekeza kuondolewa kwa nafasi ya uwakilishi wa jinsia ya kike.
“Nashukuru kwamba hapa Lamu tumeuangusha mswada wa Punguza Mizigo. Unakanganya wengi. Kwa nini kupendekeza kuondolewa kwa nafasi ya Mbunge Mwakilishi Mwanamke hapa nchini na pia vile vile nafasi zote za uteuzi? Huko ni sawa na kupiga vita jinsia ya kike na mimi binafsi siwezi kuunga mkono miswada inayokabili jinsia ya kike nchini,” akasema Bi Kale.
Mwakilihi mwingine mteule, Bw Salim Busaidy alisema mswada wa Punguza Mizigo ni wenye kupiga vita katibas na ugatuzi kwa jumla.
Alisema kupunguza nafasi za uwakilishi nchini ni sawa na kuwarudisha nyuma wakenya katika enzi ya giza.
“Katiba yetu imetoa nafasi ya ugatuzi na tayari tumejionea vile ugatuzi umesaidia mwananchi mashinani. Punguza Mizigo inapendekeza kupunguzwa kwa nafasi za wabunge na wawakilishi wengine nchini. Hilo hatuwezi kulikubali kamwe,” akasema Bw Busaidy.
Miongoni mwa kaunti ambazo kufikia sasa zimeangusha mswada wa Punguza Mizigo ni pamoja na Nairobi, Mandera, Kiambu, Nyeri, Siaya, Homa Bay, Murang’a, Nakuru, Makueni, Kirinyaga na Nyamira huku kaunti ya Uasin-Gishu ikiwa ndiyo ya pekee kupitisha mswada huo kufikia sasa.
Mswada huo wafaa kupitishwa na angalau mabunge 24 ya kaunti ili kuuwezesha kuwasilishwa kwenye bunge la kitaifa na seneti ili kupasishwa.
Ikiwa wabunge wengi zaidi katika bunge la kitaifa na seneti watapasisha mswada huo, basi utawasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ili kutiwa saini kuwa sheria.
Mswada huo unalenga kuifanyia katiba marekebisho, ikiwemo kupunguza idadi ya wabunge katika bunge la kitaifa kutoka 416 hadi 147 pekee.
Mswada huo pia unalenga kukata mishahara ya viongozi waliochaguliwa, ambapo unapendekeza mshahara wa juu uwe Sh500,000 kwa Rais wa nchi ilhali wabunge wapokee Sh300,000 kila mwezi.
Punguza Mizigo pia unapigania kuongeza mgao wa kifedha unaoelekezwa kwa kaunti kutoka asilimia 15 hadi angalau asilimia 35.