Habari

Pigo kwa afisa wa IEBC aliyefutwa kwa kushiriki kazi za pembeni

Na JOSEPH WANGUI May 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA ya kusikiza kesi zinazohusiana na masuala ya Leba imedinda kusitisha uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wa kumfuta kazi mmoja wa maafisa wake kwa kufanya kazi za ziada kuongezea mapato yake.

Bw Oyugi Omuomo alipigwa kalamu Januari 2023 baada ya kugunduliwa kuwa alikuwa akikifanyia kazi Chuo Kikuu cha Maseno, kama fundi wa masuala ya mitandao, ikiwa hayuko kazini.

Jaji Mathews Nduma Nderi alisema ombi lililowasilishwa na Bw Omuomo akiitaka mahakama hiyo kusitisha kufutwa kazi, halikuwa sawa na halingeweza kushughulikia barabara mzozo huo kuhusu kutamatishwa kwa ajira.

Hii ni kwa sababu wakati huo Bw Omuomo alifika katika mahakama hiyo ya Leba, alikuwa amekata rufaa nyingine katika Idara ya Kushughulikia Wafanyakazi ndani ya IEBC na uamuzi kuhusu rufaa hiyo ungali unasubiriwa.

“Ombi hilo si sawa lilivyowasilishwa kushughulikia masuala ya kandarasi ya utendakazi kati ya Bw Omuomo na IEBC na imefutiliwa mbali kwa misingi hiyo pekee,” Jaji Nderi akasema.

Bw Omuomo alifutwa kazi kwa kuenda kinyume na taratibu za IEBC kwa kushiriki katika kazi nyingine ya kumletea mapato.

Ilielezwa kuwa aliajiriwa, kwa misingi ya kandarasi, katika chuo hicho ilhali ameajiriwa kwa kandarasi ya kudumu katika IEBC.

Mlalamishi aliajiriwa na tume hiyo katika Idara yake ya Teknolojia na Mawasiliano (ICT) mnamo 2024.

Lakini mnamo 2017 alianza kuhudumia Chuo Kikuu cha Maseno, nyakati ambapo alikuwa likizoni, lakini baadaye akapewa kandarasi ya mwaka mmoja na taasisi hiyo ya masomo, ambayo iliongezwa miaka mitatu iliyofuata.

Bw Omuomo aliiambia mahakama hiyo kwamba kazi yake ya ziada haiathiri kwa vyovyote ajira yake katika IEBC na hajawahi kuchelewa kuripoti kazini katika tume hiyo.

Katika vikao ya kamati ya nidhamu alieleza kuwa hajawahi kukosa kufikia kazini lakini aliyekuwa Kamishina wa Abdi Guliye alimjibu kwamba huenda “ulikuwa unajitokeza kisha unaondoka.”

Mahakama iliambiwa kuwa kikao cha kamati ya nidhamu kilidumu kwa dakika tatu pekee na kwamba Omuomo hakuwepa stakabadhi yoyote iliyoonyesha kuwa alikuwa akishikilia ajira mbili kwa wakati mmoja.