Pigo kwa Gavana Waititu kuambiwa hafai kuingia afisini
Na RICHARD MUNGUTI na KENNEDY KIMANTHI
GAVANA wa Kiambu, Ferdinand Waititu, amekatazwa kuingia afisini mwake kipindi chote cha kesi ya ufisadi wa Sh588 milioni dhidi yake ambapo anadaiwa kukiuka sheria na utaratibu wa tenda miongoni mwa makosa mengine.
Ni pigo kwa Waititu ambaye ameachiliwa kwa dhamana ya Sh15 milioni, huku mkewe, Susan Wangari naye akichiliwa kwa dhamana ya Sh4 milioni.
Uamuzi umetolewa na hakimu Lawrence Mugambi.
Wengine walioshtakiwa ni mkurugenzi wa Testimony Enterprises Limited, Charles Chege ambaye naye ameachiliwa kwa dhamana ya Sh15 milioni.
Chege amewakilishwa mahakamani na wakili John Swaka.
Kizuizi hicho cha kuingia afisini kinatokana na uamuzi wa wiki jana ambapo Jaji Mumbi Ngugi katika alisema magavana wanaokabiliwa na mashtaka ya kuhujumu uchumi wanafaa kukaa kando hadi kesi zitakaposikilizwa na kuamuliwa.
Jaji Ngugi alisema magavana sawa na watumishi wengine wa umma wanafaa kukaa kando mara wakishtakiwa na makosa ya kiuhalifu na majukumu yao kuchukuliwa na manaibu wao kipindi cha kesi.
Hii inamaanisha naibu wa Waititu, Dkt James Nyoro – ambaye wamekuwa wakitofautiana – ndiye ataendesha shughuli za kaunti.