Habari

Pigo kwa Ruto jopo la fidia likiharamishwa

Na RICHARD MUNGUTI, SAM KIPLAGAT September 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JOPO lililoteuliwa na Rais William Ruto kuchunguza na kupendekeza kulipwa fidia kwa wahanga waliojeruhiwa wakati wa ghasia za maandamano na dhuluma za polisi limepata pigo kubwa baada ya Mahakama Kuu kusitisha utendakazi wake.

Jaji Dennis Kizito Ngw’ono Mongare alipiga breki jopo hilo linaloongozwa Mtaalamu wa masuala ya kisheria Profesa Makau Mutua hadi pale kesi iliyowasilishwa na wakili Levi Munyeri itakaposikizwa na kuamuliwa.

Jaji Mong’are alisitisha kazi ya jopo hilo lililoteuliwa wiki iliyopitaa hadi Oktoba 10,2025 kesi hiyo itakaposikizwa.

Jaji huyo aliratibisha kuwa ya dharura kesi hiyo iliyoshtakiwa na Bw Munyeri anayedai Rais Ruto aliukiuka sheria kuteua jopo hilo kabla ya wahasiriwa kujulikana na majeraha waliyopata kutathminiwa na watalaam wa afya.

Mnamo Agosti 25 2025 Rais Ruto aliteua jopo la wanachama 14 akiwamo Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Faith Odhiambo kuchunguza na kubaini idadi ya watu waliopigwa risasi na polisi na kujeruhiwa.

Haya yalitokea wakati wa maandamano ya kupinga sheria ya Fedha 2024/2025 na wakati wa kumbukumbu ya wahasiriwa wa dhuluma za polisi wa Juni 18/20.2024.

Mbali na wahasiriwa hao wa hivi majuzi pia jopo hilo lilitwikwa jukumu la kuwatambua wahasiriwa wa waamandamano ya hapo awali kwa lengo la kuwalipa fidia.

RaiS aliitaka jopo hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kisheria, litoe mapendekezo ya kiwango cha pesa amabazo wahasiriwa watalipwa na wakati huo huo kutoa mapendekezo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuhusu wale wanaopasa kufunguliwa mashtaka kortini.

Wakati huo huo mahakama imepiga breki matumizi ya zabuni ya elektroniki kwa asasi za serikali na serikali za kaunti jinsi ilivyoamrishwa na Rais William Ruto.

Jaji Bahati Mwamuye alitoa amri ya kuzuia matumizi ya mfumo wa utoaji zabuni kwa njia ya elektroniki maarufu kama e-Gp hadi kesi iliyowasilishwa na Baraza la Magavana Nchini (CoG) na watu wengine wanne isikizwe na iamuliwe.

Waliowasilisha kesi walikuwa wakisema hakukuwa na mikutano ya ushirikishaji wa umma jinsi inavyotakikana kwenye katiba na pia serikali za kaunti hazikushauriwa.

CoG ilisema utoaji wa zabuni kwa njia ya elektroniki ni sawa ila mtandao unaotumika haufai kuundwa haraka na utekelezaji kukumbatiwa.

“Natoa amri ya kumzuia waziri wa fedha kukumbatia matumizi ya lazima ya e-GPS katika shughuli zote za utoaji zabuni wa serikali,” ikasema amri ya Jaji Mwamuye.

Jaji aliamrisha kesi hiyo isikizwe mnamo Oktoba 14