POLENI! Wafanyakazi 1,529 kupoteza ajira serikali ikivunja mashirika 6 ya kikanda
WAFANYAKAZI 1,529 watapoteza nafasi zao za ajira na miradi 429 kukwama ikiwa serikali itavunja mamlaka sita za ustawi wa kikanda (RDAs), afisi inayoshauri kuhusu masuala ya bajeti bungeni (PBO) imeonya.
Wizara ya Fedha inapania kuvunja mamlaka hizo zenye mali ya thamani ya Sh4.9 bilioni kwa sababu majukumu yao yanaingiliana na yale ya serikali za kaunti.
Hii ni sehemu ya mchakato ulioanzishwa na wizara hiyo kuyafanyia marekebisho Mashirika ya Serikali ili kulainisha utendakazi wa asasi hizo.
Mamlaka hizo sita za Kikanda ni kati ya asasi 90 zinazofanyiwa marekebisho kupitia kuunganishwa, kubinafsishwa na kuvunjwa, serikali kuu inapojizatiti kuokoa fedha za umma na kuimarisha shughuli za asasi zake.
“Hata hivyo, hatua ya kuvunjwa kwa mamlaka hizo za kikanda huenda ikakumbwa na changamoto kwa sababu zinaendesha jumla ya miradi 423. Miongoni mwa miradi hiyo inatekelezwa katika maeneo yanayovuka mipaka ya zaidi ya kaunti moja,” PBO ikasema
“Kando na mali ya thamani kubwa, mamlaka hizo zimeajiri jumla ya wafanyakazi 1,529 ambao mishahara na marupurupu yao inagharimu karibu Sh1.53 bilioni,” afisi hiyo inaongeza.
PBO ambayo pia hutoa ushauri wa kitaalamu kwa bunge kuhusu masuala ya kiuchumi, inaonya kuwa kuvunjwa kwa mamlaka hizo za kikanda bila mpango wa namna ya kushughulikia wafanyakazi, mali na miradi, huenda ukakumbwa na changamoto za kisheria.
Mamlaka hizo sita ni; Mamlaka ya Maendeleo ya Mito Tana na Athi, Mamlaka ya Maendeleo la Bonde la Kerio, Mamlaka ya Maendeleo ya Eneo la Ziwa, Mamlaka ya Maendeleo ya Ewaso Ng’iro Kusini na Mamlaka ya Maendeleo ya Ukanda wa Pwani.
“Kuvunjwa kwa mamlaka hizo kutaathiri miradi na usimamizi wa miradi inayoendelea na usimamizi wa mali na madeni katika asasi hizo,” PBO inasema
Serikali ya Kitaifa inalenga kufanya marekebisho kwa Mashirika yake kwa kuunganisha mashirika 42 hadi kusalia 20, kuvunja mashirika tisa, kuunda upya mashirika sita, kubinafsisha au kuvunja mashirika 16 ambayo majukumu yao yamepitwa na wakati.
Serikali kuu pia inalenga kuorodheshwa upya hazina 17 na mashirika ya kitaalamu yanayoanishwa kama Mashirika ya Serikali.
Mashirika hayo 90, kwa pamoja, yalitengewa bajeti ya kima cha Sh122 bilioni katika mwaka huu wa kifedha na PBO inasema kiasi kikubwa cha pesa kitaokolewa kutokana na marekebisho yanayoendeshwa na serikali.
“Hata hivyo, manufaa ya kiuchumi kutoka kwa mashirika haya ya serikali yamekuwa duni ikilinganishwa na fedha yanazotumia.
Hii ni kutokana na mwingiliano wa majukumu yao, muundo sawa wa usimamizi na utoaji huduma usiolainishwa,” inaeleza PBO.
Aidha, mashirika mengi yalilengwa kufanyiwa mageuzi kwa sababu hayazalishi pesa kivyao bali hutegemea pakubwa ufadhili kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.
Mashirika yanayolengwa kubinafsishwa ni Wakfu wa Jomo Kenyatta, Kampuni ya Kusindika Pareto Nchini (PPCK), Numerical Machining Complex na Benki ya Posta.