Habari

Polisi wafaulu kuzima makali ya maandamano kwa kukabili makundi ya vijana mapema

Na WAANDISHI WETU July 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MJI wa Karatina ambao umekuwa kitovu cha maandamano Kaunti ya Nyeri Jumatatu ulisalia mahame kuanzia saa moja asubuhi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saba Saba.

Biashara zilisitishwa, benki zikifungwa huku safari za kuingia au kutoka kwenye mji huo zikizimwa.

Shule nazo zilifungwa wakati vijana nao walizima shughuli za uchukuzi kwenye barabara ya Karatina-Nairobi. Barabara hiyo pia huunganisha Nairobi na Kaskazini Mashariki pamoja na mji wa Nanyuki.

Maandamano yalianza saa moja asubuhi vijana wakiwasha moto barabarani, wakipuliza kipenge na kusema ‘muhula moja’.

Polisi waliingia barabarani saa tatu unusu na kuanza kuwafurusha waandamanaji ambao waliwatupia mawe na makabiliano yakaanza.

Mjini Nyeri, kulikuwa na taharuki asubuhi kabla ya polisi kuanza kukabiliana na waandamanaji saa tano mchana. Polisi walitumia vitoza machozi kuwakabili vijana ambao walijaribu kuingia katikati mwa mji huo.

Kufikia saa sita na nusu mchana vijana bado walikuwa wakikabiliana na polisi Karatina lakini kulikuwa na utulivu eneo la Nyeri.

Miji ya Embu na Ngurabani Kaunti ya Kirinyaga, polisi waliwatawanya waandamanaji na kuwakabili kwa vitoza machozi.

Waandamanaji hao walikuwa wameziba barabara ya Embu-Makutano na kuwasha moto barabarani nyakati za asubuhi. Hali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa.

Fujo zilitawala makabiliano kati ya polisi na waandamanaji ambao walionekana hawakuwa tayari kuondoka barabarani.

Mjini Murangá, mamia ya waandamanaji waliziba mpaka wa kaunti hiyo na Kirinyaga eneo la Sagana.

Kulikuwa na vizuizi vingi vilivyowekwa na vijana ambao walikuwa wakiwatoza pesa waliokuwa wakitumia magari barabarani humo.

Mji wa Maua Kaunti ya Meru haukuachwa nyuma, baadhi ya waandamanaji wakiwasha moto na kuwatupia polisi mawe.

Ripoti za Stephen Munyiri, Mercy Mwende, George Munene, Mwangi Muiruri na David Muchui