Polisi walikiuka katiba kutumia ukatili dhidi ya Gen Z- Korti yashikilia
MAHAKAMA Kuu imeshikilia kuwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ilikiuka Katiba kwa kutumia nguvu kupita kiasi, zikiwemo risasi halisi, risasi za mpira na gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji wa kizazi cha Gen Z waliokuwa wakipinga Mswada wa Fedha wa 2024 kwa amani.
Katika uamuzi wa kihistoria wenye athari kubwa kwa uwajibikaji wa polisi na haki za kuandamana, Jaji Mugure Thande alilaani hatua za polisi akisema ni “za kikatili, kupita kiasi na kinyume cha Katiba,” ambazo zilisababisha vifo, majeraha, na kukamatwa kiholela kwa waandamanaji.
Jaji Thande alitangaza kuwa matumizi ya maji ya mwasho, gesi ya kutoa machozi, na risasi dhidi ya raia wasio na silaha ni kinyume cha Katiba.
“Polisi walitenda zaidi ya kile wanachoruhusiwa kwa mujibu wa Katiba na sheria,” alisema.
Aidha, alisema kwamba polisi walishindwa kutumia mbinu zisizo za nguvu kama inavyotakiwa kisheria.
Pia alikosoa matumizi ya maafisa waliovaa barakoa na magari yasiyo na nambari za usajili wakati wa maandamano jambo linaloenda kinyume na maadili ya uwazi na uwajibikaji.
Jaji aliuliza, “Kwa kuwa jukumu lao ni kuhudumia wananchi wote, kwa nini polisi wafiche sura zao na utambulisho wao na kuwakamata watu kwa magari yasiyotambulika?”
Aliongeza, “ni wahalifu tu wanaojificha kwa kuvaa kofia na barokoa na kutumia magari bila nambari ili wasijulikane. Kwa nini polisi wajifananishe na wahalifu?”
Mahakama ilisema kuwa visa vya utekaji nyara, mateso na unyanyasaji wa waandamanaji vilikiuka haki za msingi zilizoainishwa katika Ibara ya 26 (haki ya kuishi), Ibara ya 29 (uhuru dhidi ya mateso), na Ibara ya 37 (haki ya kuandamana kwa amani).
Uamuzi huu ulitolewa baada ya kesi iliyowasilishwa na wakili Saitabao Ole Kanchory, ambao pia ilibainika kuwa kulikuwa na pengo kubwa la uwajibikaji miongoni mwa maafisa wa usalama.
Katika ushahidi wake, Kanchory alieleza kuwa waandamanaji wa Gen Z walikumbwa na ukatili mkubwa licha ya kuandamana kwa amani kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.
Ripoti za Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) zilibainisha kuwa polisi walitumia risasi na gesi ya kutoza machozi bila kujali, hata kwa maeneo ya huduma za kwanza kama vile kambi za matibabu mnamo Juni, Julai na Agosti 2024.
Katika hati ya kiapo ya Abdirahman Jibril, Mkurugenzi Msaidizi wa Uchunguzi wa IPOA, ilibainika kuwa polisi hawakutekeleza wajibu wao wa kuwezesha maandamano kwa mujibu wa Ibara ya 37 ya Katiba.