Habari

Polisi waumia ripoti ikionyesha wametengewa washauri nasaha wachache

Na ERIC MATARA November 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RIPOTI mpya imeonyesha kuwa maafisa wa polisi huwa hawapokei huduma za ushauri nasaha ndio maana wamekuwa wakilemewa na msongo wa mawazo.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi wa mitandao, sera na majukumu ya Tume ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPSC) ambayo inalenga kumaliza ufisadi, kuimarisha utoaji wa huduma na pia kuwianisha utendakazi wa maafisa wa polisi.

Ukaguzi huo umeonyesha kuwa polisi wamekuwa wakiumia kwa sababu hakuna idadi tosha ya watoaji ushauri nasaha katika NPS.

Maafisa hao ni wachache sana katika kaunti, kaunti ndogo, vituo vya polisi na taasisi za mafunzo huku idadi ya maafisa wa polisi wakiwa wengi.

“Ripoti hiyo imeanika kuwa Kaunti ya Kisii ina mtoaji ushauri nasaha mmoja pekee na aliwashughulikia zaidi ya polisi 70 kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Aprili 28, 2025,” ikasema ripoti hiyo ya ukaguzi.

“Kati ya kazi ambazo alifanya ni kutoa ushauri kwa wale waliofiwa, waliokuwa na changamoto mbalimbali kazini, msongo wa mawazo na wale ambao walikuwa na uraibu wa kutumia dawa za kulevya,” ikaongeza ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ukaguzi, ni washauri wawili pekee ndio wako katika Kaunti ya Isiolo kuwahudumia maafisa wa polisi.

“Katika baadhi ya matukio NPS haikutoa hela ya kugharimia nauli ya washauri na watoaji nasaha jinsi ilivyokuwa Isiolo. Hii ni licha ya polisi wa eneo hilo kukumbana na changamoto nyingi walipokuwa wakiendelea na kazi zao,” ikasema ripoti ya ukaguzi.

Akiwa mbele ya Kamati ya Bungu kuhusu Uwiano, Afisa Mkuu Mtendaji wa NPS Peter Leley alisema kuwa idara hiyo kwa sasa haina maafisa wa kutosha wa kutoa ushauri na nasaha.

Alisema vituo vya utoaji ushauri na nasaha ni vipo katika maeneo manane huku polisi kutoka kaunti za Samburu, Turkana, Pokot Magharibi na Baringo wakiwa hawasaidiwi. Hii ni licha ya kwamba maeneo haya ndiyo hukumbana na visa vya ujangili na wizi wa mifugo.