Raila akataa kudokeza iwapo atamuunga mkono Dkt Matiang’i
KINARA wa ODM Raila Odinga Alhamisi alikataa kubainisha iwapo atamuunga mkono aliyekuwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i katika azma yake ya kuwania urais mwaka wa 2027 au la.
Mwanasiasa huyo mkongwe, alisema Dkt Matiang’i hajatangaza iwapo atawania urais kwa hivyo ni vigumu kwake kulizungumzia suala hilo.
Dkt Matiang’i amekuwa akipigiwa upatu na Wakenya mbalimbali, hasa vijana wa Gen-Z, kama kiongozi mfaafu, anayefaa kupewa jukumu la kuliongoza taifa hili kutokana na utendakazi wake mzuri alipohudumu katika serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Wakenya hao wametamauka na utawala wa Kenya Kwanza, wakiulaumu pakubwa kwa kukosa kutimiza ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.
Akiongea jana alipozuru Kaunti ya Kisii, baada ya mkutano na wafuasi wa chama chake kutoka eneo hilo, Bw Odinga alidokeza kuwa kwa sasa amejikita katika mashauriano na washirika wake kuhusu mwelekeo wa kisiasa atakaouchukua baada ya kupoteza kiti cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
“Matiang’i hajajitokeza na kusema anautafuta urais katika uchaguzi mkuu ujao. Ili uchaguliwe rais, mwaniaji hatahitaji tu kura za jamii anayotoka bali kura za Wakenya kwa jumla,” Odinga alisema.
Kwenye ziara hiyo, Bw Odinga aliwataka Wakenya wawe na subira kuhusu tangazo la mwelekeo wake.
Kinara huyo wa upinzani pia aliitaka serikali ya Rais William Ruto kushughulikia malalamishi yanayoibuliwa na Wakenya kama vile utata unaozunguka Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) na ufisadi miongoni mwa masuala mengine.
Kuhusu machafuko yanayoendelea katika mpaka wa kaunti za Kisii na Narok, katika eneo la Kiango, Bw Odinga alivitaka vyomba vya usalama kuhakikisha hali ya utulivu inarejea kwa kukomesha visa vya wizi wa mifugo.