Habari

Raila alamba sakafu seneti

July 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amepata pigo baada ya maseneta kutoka ngome zake za kisiasa kumkaidi na kupinga mfumo mpya wa ugavi wa fedha baina ya kaunti ambao unazingatia zaidi idadi ya watu.

Orodha ya jinsi maseneta walivyopiga kura kuhusu suala hilo Jumanne usiku, imeonyesha kati ya vigogo wakuu wa kisiasa nchini, Bw Odinga ndiye alipata pigo zaidi.

Sababu ni kwamba, maseneta wengi wa Mlima Kenya waliunga mkono mfumo huo alivyopendekeza Rais Uhuru Kenyatta, huku wale wa Rift Valley wakiupinga.

Eneo la Mlima Kenya ni ngome ya Rais Kenyatta, na Rift Valley ni ngome ya naibu wake, Dkt William Ruto, ambaye wafuasi wake wamekuwa wakimkaidi Rais kwa muda mrefu sasa.

Maseneta wa ODM kutoka Pwani na kaunti zingine isipokuwa Luo Nyanza walikuwa miongoni mwa maseneta 25 waliopinga mfumo huo wa Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) kwa misingi kwamba, kaunti maskini zitapoteza mabilioni ya pesa.

Msimamo wa maseneta hao wa ODM ni pigo kwa mustakabali wa kisiasa wa Bw Odinga ikizingatiwa kuwa, atategemea uungwaji mkono kutoka maeneo hayo kufanikisha ndoto yake ya kuingia Ikulu 2022.

Maseneta wa Pwani, ambao ni Mohammed Faki (Mombasa), Stewart Madzayo (Kilifi), Isaa Juma Boy (Kwale), Jonnes Mwaruma (Taita Taveta), Ali Wario (Tana River) na Anuar Loitiptip (Lamu) wote walimkaidi Bw Odinga.

“Suala hili halihusiani na misimamo ya vyama au viongozi fulani. Hili ni suala linalohusu masilahi ya wananchi waliotutuma katika bunge hili kutetea masilahi yao. Kwa hivyo, sisi kama Wapwani hatuwezi kuunga mfumo huo unaotupokonya fedha hata kama utatekelezwa baada ya miaka miwili,” akasema Bw Madzayo.

Alitamka hayo alipopinga pendekeza la Kiranja wa Wengi, Irungu Kang’ata, kuwa utekelezaji wa mfumo huo uanze mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

Msimamo huo pia uliungwa mkono na maseneta Ledama Ole Kina (Narok, ODM) na Cleopas Malala (Kakamega, ANC) ambao pia ni wandani wakuu wanaotegemewa kuvumisha misimamo ya Bw Odinga nje na ndani ya Seneti.

“Ingawa kaunti yangu ya Kakamega itaongezewa Sh800 milioni chini ya mfumo huu, naupinga kwa sababu unaligawanya taifa hili. Siwezi kuunga mkono mfumo huu utakaopelekea wenzetu kutoka Pwani, Kaskazini na eneo la Kisii kuhisi kutengwa,” akasema Bw Malala.

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Seneta wa Kisii Sam Ongeri ambaye pia aliupinga licha ya kwamba kaunti yake ilitarajiwa kupata nyongeza ya Sh220 milioni.

“Nasimama na jirani yangu wa Nyamira Okong’o Omogeni kupinga mfumo huu ambao unahujumu umoja wa kitaifa,” Profesa Ongeri akasema. Kaunti ya Nyamira itapoteza Sh650 milioni chini ya mfumo huo.

Mnamo Jumatatu, Bw Odinga aliwataka maseneta kupitisha mfumo huo ambao wanaoupinga wanasema ungedhulumu kaunti za Pwani, Kaskazini mwa Kenya na Ukambani kwani ungetegemea ugawaji kwa msingi wa wingi wa watu badala ya ukubwa wa eneo.

Katika mrengo wa Jubilee, mgawanyiko ulionekana kati ya wanaoegemea upande wa Rais Kenyatta na wandani wa Dkt Ruto lakini pia baadhi ya wandani wa Rais wakakaidi agizo lake.

Waliopinga mfumo huo ni Kipchumba Murkomen (Elgeyo-Marakwet), Johnson Sakaja (Nairobi), Fatuma Dullo (Isiolo), Kindiki Kithure (Tharaka Nithi), Ltumbesi Lelegwe (Samburu), Philip Mpaayei (Kajiado), Mahamud Mohamed (Mandera) miongoni mwa wengine.

Maseneta wa Ukambani Enoch Wambua (Kitui), Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na Boniface Kabaka (Machakos) pia walimkaidi kinara wao Kalonzo Musyoka aliyeunga mkono mfumo huo.

Kiongozi huyo wa Wiper alikuwa amebaliana na msimamo wa Bw Odinga kwamba, “pesa hunuiwa kuboresha maisha ya watu.”

Jumaane wiki ijayo, maseneta wataendelea kujadili mfumo mpya uliopendekeza na Bw Sakaja ambao anasema, unalenga kuhakikisha hakuna kaunti itakayopoteza fedha zozote.