Habari

Raila aliibiwa kura 2022 baada ya sajili kuvurugwa, asema SK Macharia

Na PIUS MAUNDU March 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANDANI wa Kinara wa ODM Raila Odinga amesema njia pekee ya kuhakikikisha kuwa kuna uchaguzi mkuu mnamo 2027 ni kusafisha sajili ya wapigakura.

Samuel Kamau Macharia, mmiliki wa Kampuni ya Royal Media Services amesema kuwa tatizo ambalo limekuwepo katika chaguzi za nyuma ni sajili feki kutumika kumpokonya Bw Odinga ushindi.

“Mnamo 2022, tulienda Naivasha kuweka mikakati ya kuhakikisha Raila anashinda kura. Nilijaribu kufafanua kuwa sajili ya wapigakura iliyokuwa ikitumika ilikuwa feki lakini Raila hakuwa na subira nami,” akasema Bw Macharia.

“Alikuwa na imani kuwa handisheki na Rais Uhuru Kenyatta ingemsaidia. Makamishina waasi ambao walitimuliwa walikuja nyumbani kwangu na nikawaonyesha jinsi sajili iliyotumika ilikuwa feki. Hiyo pamoja na suala la Chris Msando, ndivyo uchaguzi ulivurugwa na kura kuibwa,” akaongeza.

Alikuwa akizungumza Maanzoni Machakos wakati wa mazishi ya Kanali Mstaafu James Gitahi, ambaye alifariki wiki mbili zilizopita kwenye ajali ya barabarani.

Marehemu alipata umaarufu sana kwa kuwa rubani wa ndege zilizotumika na Marais Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki. Bw Gitahi ni mumewe Seneta Mteule Betty Montet.

Bw Msando aliuawa siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Pia aliwarejelea waliokuwa naibu mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Juliana Cherera na makamishina Francis Wanderi, Justus Nyangáya na Irene Masit.

Makamishina hao walitofautiana na aliyekuwa Mwenyekiti wa IEBC marehemu Wafula Chebukati na makamishina Boya Mulu na Prof Abdi Guliye kuhusu mshindi wa uchaguzi mkuu uliopita.

Bw Macharia alisema kuwa Raila amekuwa akishinda kura nchini lakini anaibiwa huku akisema yupo tayari kwa lolote nia yake kuu ikiwa ni kuwahakikisha Kenya inaandaa chaguzi huru.

“Nina miaka 84 kwa hivyo hata nikitekwa nyara au kukamatwa si hoja. Ningependa kumwaambia Rais Ruto kuwa akitaka kuacha nchi vizuri, iwe alichaguliwa kwa halali au la ,anastahili kuwacha sajili safi ya wapigakura,” akasema Bw Macharia.

“Hii ndiyo njia pekee ambapo Wakenya watapiga kura kwa haki. Na hata akipoteza, ataiacha nchi ambayo mshindi halali amepatikana,” akasema.

Bw Odinga aliunga kauli ya Bw Macharia ambapo alisema ni uchaguzi wa 2002 pekee ndio ulikuwa huru na mshindi halali akapatikana.

“Nyote mnajua kilichotokea kwenye chaguzi zote zilizopita jinsi ambavyo Bw Macharia amewaambia. Umesema unataka nishinde lakini nimeshinda mara nyingi ila tu sijatangazwa,

“Hiyo ndiyo maana nimekuwa nikiwashinikiza wafungue sava ya IEBC. Uliwaona wakifungua?” akauliza.

Wakati wa mazishi hayo Raila alitetea ushirikiano wake na Rais Ruto akimpuuza Seneta wa Murangá Joe Nyutu aliyemtaka afanye kazi na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

“Wakenya wanahitaji kuishi kuanzia sasa hadi 2027, Kenya ni kubwa kutuliko na demokrasia ni mchakato. Hakuna haja ya kuniambia niwanie 2027 kama nchi itakuwa pabaya na imesambaratika,” akasema Bw Odinga.

Alisema muafaka wake na Rais Ruto itasaidia kupunguza gharama ya maisha, kupunguza ushuru na ufisadi ambao umeongezeka serikalini.