Habari

Raila alijtambulisha na madhehebu tofauti

Na Elvis Ondieki October 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

INGAWA Kanisa la Anglikana limepewa jukumu la kuongoza mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, ukweli ni kwamba marehemu hakuwa akijitambulisha waziwazi na dhehebu hilo wakati wa maisha yake.

Kwa muda mrefu, Raila alionekana kuwa mtu wa imani nyingi — mara akiwa kwenye mavazi ya Kiislamu, mara akishiriki ibada na waumini wa Legio Maria au madhehebu mengine mbalimbali, kulingana na mazingira au hafla.

Hata hivyo, siku ya Jumatano baada ya kifo chake, kamati ya maandalizi ya mazishi ilitangaza rasmi kuwa ibada ya mwisho ya kumuaga Odinga itasimamiwa na Kanisa la Anglikana.

“Mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga yatafanyika siku ya Jumapili na yataongozwa kwa taratibu za Kanisa la Anglikana, ambalo alikuwa muumini,” alisema mwenyekiti wa kamati hiyo, Prof Kithure Kindiki.

Lakini si kila mtu anakumbuka kwamba miaka 16 iliyopita, Raila alibatizwa upya na Nabii David Owuor wa Kanisa la Toba na Utakatifu. Mnamo  Mei 4, 2009, akiwa Waziri Mkuu, Raila alitumbukizwa ndani ya kidimbwi cha kuogelea katika Riverside Drive jijini Nairobi, mbele ya kamera na watu wakishuhudia.

Hata hivyo, haijawahi kufahamika wazi iwapo ubatizo huo ulimfanya ahamie kabisa katika dhehebu la Owuor au lilikuwa tukio la kipekee la wakati huo.

Leo hii, akiwa ameaga dunia, ni Kanisa la Anglikana litakaloongoza safari yake ya mwisho  ishara ya ushawishi na nafasi yake katika jamii nyingi za kidini alizojihusisha nazo kwa miongo mingi.