Raila guu moja ndani, jingine nje; asema bajeti ya Mbadi ni nafuu
KINARA wa upinzani Raila Odinga Jumanne aliendelea kuwakanganya wafuasi wake kwa kusema kwamba hayuko serikalini na wakati huo huo akatoa wito wa kuungwa kwa mawaziri wa ODM ambao wanatumikia utawala wa Kenya Kwanza.
Bw Odinga amekuwa akilazimika kutumia majukwaa mbalimbali kujitetea kuwa ODM si sehemu ya utawala wa Rais William Ruto ambayo inakabiliwa na maasi hasa kutoka kwa Gen Z.
Akiongea wakati wa mkutano wa uhasibu jijini Mombasa, Bw Odinga aliwataka wanasiasa kuunga mkono ‘wataalamu’ wa ODM ambao wanahudumu kama mawaziri akisema kuwa watasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.
Baadhi ya viongozi wa ODM ambao wanahudumu kama mawaziri ni John Mbadi (Fedha), Opiyo Wandayi (Kawi), Hassan Joho (Madini), Beatrice Askul (Jumuiya ya Afrika Mashariki) na Wycliffe Oparanya (Vyama vya ushirika na biashara ndogo ndogo).
Hasa alisema bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2025/26 itakuwa nafuu na itachangia kuleta mabadiliko ya kiuchumi kutokana na uongozi wa kuridhisha wa Bw Mbadi.
“ODM ilisadia serikali na wataalamu na ilikuwa tu Julai mwaka jana. Sasa tupo Mei, hawajafanya bajeti yote na bajeti ya Mbadi mwaka huu ndiyo itatumika kutathmini utendakazi wake, kwa hivyo, mpeni wakati na mtaona tofauti,” akasema Bw Odinga.
“Wape wataalamu wa ODM muda wa kufanya kazi na mtaona matunda yake,” akaongeza akijibu maswali kutoka kwa Wakenya wakati wa kikao hicho.
Hii ni mara nyingine ambapo Bw Odinga anasisitiza kuwa hayupo serikalini na kuwakanganya wafuasi wake ikizingatiwa baadhi ya viongozi wa ODM wamekuwa wakisisitiza wapo na Rais Ruto sako kwa bako.
Mnamo Jumamosi, Bw Odinga akihudhuria mazishi ya jamaa yake Siaya, alitofautiana na nduguye Dkt Oburu Oginga, akisema kuwa hayuko serikalini.
“Oburu anaongea tu maneno ambayo hayapo, mimi siko serikalini, niko nje. Wacha waongee,” akasema Raila akiunga mkono kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Gavana James Orengo za kukosoa serikali.
Akiwa Mombasa, Bw Odinga kwa mara nyingine aliwakemea wabunge kuhusu kusimamia Hazina ya Fedha ya Ustawi wa Maeneobunge (CDF) akisema kuwa hazina hiyo inastahili kusimamiwa na magavana kwenye kaunti.
Pia alisema ada ya ujenzi wa barabara mashinani inafaa ielekezwe kwa kaunti badala ya kusalia na serikali kuu huku akisisitiza kazi wabunge ni kutunga sheria na kufuatilia matumizi ya rasilimali za serikali.
“Sasa wanafanya mikutano ya kushirikisha umma, wafanye mingi jinsi wanavyoweza lakini tukienda kura ya maamuzi watapoteza,” akasema.
Hata hivyo, alisema magavana ambao ni wafisadi wanastahili kuchukuliwa hatua kali za kisheria.