Habari

Raila kuongoza kikao kuamua mgombea wa ODM Kibra

August 21st, 2019 2 min read

Na SAMWEL OWINO na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga anatarajiwa Ijumaa kuongoza mkutano wa Kamati Kuu ya Usimamizi (CMC) ya chama hicho kuamua mfumo utakaotumiwa kuteua mgombeaji wake katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) tayari imetangaza kuwa uchaguzi huo utafanyika Novemba 7, 2019, na vyama vinavyonuia kudhamini wagombeaji vimepewa makataa ya hadi Septemba 10 kukamilisha uteuzi.

Bw Odinga, ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundomsingi, anatarajiwa kurejea nchini Ijumaa kutoka ziara ya kikazi nchini Indonesia ambako alihutubia kongamano moja kuhusu miundomsingi.

Kamati ya CMC inayumuisha kiongozi wa chama, mwenyekiti na manaibu wake wawili, katibu mpanga ratiba, Katibu wa masuala ya vijana, katibu wa masuala ya vijana na katibu wa masuala ya bunge.

ODM inatarajiwa kuamua iwapo kati ya mifumo mitatu ya uteuzi wa atakayewania kiti hicho kilichobaki wazi kufuatia kifo cha Ken Okoth mwezi jana, baada ya kuugua kansa ya utumbo.

Wanachama wa kamati hiyo watachagua kati ya mbinu ya uteuzi kwa njia ya maelewano, upigaji kuwa wa moja kwa moja, au kupeana tiketi ya moja kwa moja kwa mgombeaji wanayempendelea.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi jana alithibitisha uwepo wa mkutano huo akisema ODM itateua mbinu bora ambayo haitawaacha wanachama wake wakilalamika au kudai kutotendewa haki.

“Siwezi nikasema sasa ikiwa chama kitaamua kutumia mbinu ya uteuzi wa moja kwa moja au la. Ni suala ambalo litajadiliwa na kuamulia Ijuma. Lakini mbinu itakayokubali ni ile itafaa chama na wafuasi wake,” Bw Mbadi akaambia Taifa Leo.

Mnamo Jumanne chama cha ODM kilitoa ujumbe kwa wagombeaji wote kuchukua fomu za uteuzi katika makao makuu, wazijaze na kuzirejesha kufukia Ijumaa.

“Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) inatoa notisi kwa watu wote wenye nia ya kushiriki uteuzi wa kuwa mgombeaji wa ODM katika uchaguzi mdogo wa Kibra kuchukua fomu za maombi kutoka makao makuu jumba la Orange au katika tovuti yake. Wazijaze na kuzirejesha katika makao makuu ifikapo Ijumaa Agosti 23,” ikasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na mwenyekiti wa bodi hiyo Bi Judy Pareno.

Kufikia Jumatano saa kumi za jioni, watu tisa walikuwa wamefika katika jumba la Orange kuchukua stakabadhi hizo.

Hata hivyo, idadi ya waliozipakua fomu hizo kutoka tovuti ya ODM haikujulikana.

Baada ya kupokea fomu za maombi NEB itakutana Jumamosi kuwapiga msasa wagombeaji hao.

Baadhi wa watu ambao wanapania kumrithi marehemu Okoth kwa tiketi ya ODM ni pamoja na Bw Imran Okoth (kakake marehemu), Irshad Sumra (aliyekuwa Mbunge wa Embakasi Kusini), kiongozi wa vijana wa ODM eneo la Kibra Benson Musungu, Katibu Mpanga Ratiba wa ODM eneobunge la Kibwa Sigar Agumba na aliyekuwa Diwani wa wadi ya Sarang’ombe Owino Kotieno.

Mwingine anayemezea mate kiti hicho kwa chama kingine ni aliyekuwa msaidizi wa Bw Odinga Eliud Owalo.

Majuzi mwanasiasa huyo, aliyewania kiti hicho katika uchaguzi wa 2017 na akashindwa katika ngazi ya mchujo, alijiuzulu kutoka ODM.