Raila kutua Kisii, Nyamira 'kufuta nyayo za Ruto'
Na CHARLES WASONGA
KIONGOZI wa ODM Raila Odinga anatarajiwa kuzuru kaunti za Kisii na Nyamira kuanzia Jumanne, Septemba 15, 2020, kuuza ajenda ya mpango wa maridhiano (BBI) na azma yake ya kuwania urais 2022.
Ziara ya Bw Odinga katika eneo la Gusii inajiri juma moja baada ya Naibu Rais William Ruto kuzuru Kaunti ya Kisii ambapo aliongoza shughuli za michango ya fedha kuyasaidia makundi ya vijana na akina mama katika maeneobunge ya Kitutu Chache Kusini na Mugirango Kusini.
Naibu Rais ameanzisha mkakati wa kuvamia maeneo ambayo yanasawiriwa kuwa ngome za Bw Odinga katika juhudi za kuimarisha azma yake ya kuingia Ikulu.
Bw Odinga amekuwa katika ziara ya kisiasa katika eneo la Pwani kwa siku tatu ambapo alihutubia mikutano ya hadhara katika kaunti za Taita Taveta, Kwale na Mombasa. Alifanya ziara hiyo siku chache baada ya Dkt Ruto kuzuru eneo hilo haswa kaunti za Taita Taveta na Mombasa
Duru za ODM ziliambia Taifa Leo kwamba Bw Odinga alipanga ziara ya haraka eneo la Kisii kutokana na umati mkubwa wa watu waliojitokeza kwenye mikutano ya Dkt Ruto eneo hilo na kauli za wandani wake walioitaja mikutano hiyo kama ishara ya kung’aa kwa nyota yake.
Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi, Mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro na mwenzake wa Mugirango Magharibi Vincent Kemosi walisema kujitokeza kwa watu wengi katika mikutano ya Dkt Ruto ni ishara ya kuimarika kwa ufuasi wake.
“Wapi wale wanaodai kuwa Kisii ni ngome ya ODM? Wako wapi? Leo tumethibitisha kuwa eneo hili linaunga mkono kiongozi ambaye amejitolea kuwafanyia kazi Wakenya sio yule ambaye hutoa ahadi tasa. Tutashirikiana na Naibu Rais hadi mwisho,” akasema Bw Maangi, kauli ambayo iliungwa mkono na wabunge Osoro na Kemosi.
Kwa upande wake, mwanasiasa na mfanyabiashara Don Bosco Gichana alisema kuwa Naibu Rais sasa amedhibiti eneo la Gusii kisiasa.
“Raila atakuwa na kibarua kikubwa kuwashawishi wakazi wa Kisii na Nyamira kumuunga mkono kwa sababu tayari wamefanya uamuzi wa kumfuata Dkt Ruto,” akasema.
Umati uliomlaki Dkt Ruto mjini Kisii ulimzuzua aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale akasema kupitia Twitter: “Hii sio Eldoret. Hii ni Kisii na mambo bado. Dkt Ruto anawachangamsha wananchi kiasi kwamba Raila na Ogwae (Gavana wa Kisii) wameingiwa na wasiwasi. Mashinani DP anapendwa.”
Wandani wengine walioshabikia ziara hiyo ya Dkt Ruto Kisii ni aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Nakuru Susan Kihika, Seneta Maalum Millicent Omanga, Seneta wa Meru Mithika Linturi na Mbunge wa Soy Caleb Kositany.