Raila: Magavana wasiulizwe maswali na Seneti, waachwe wachape kazi
WAZIRI Mkuu wa zamani Raila Odinga amewakashifu maseneta kutokana na mtindo wao wa kuwaagiza magavana kufika mbele ya kamati zao kuwajibikia matumizi ya pesa za umma, akisema huo ni wajibu wa mabunge ya kaunti.
Bw Odinga, ambaye ni kiongozi wa ODM jana alitaja mwenendo huo kama wa kupoteza muda na pesa za umma, akiwataka maseneta kuwaacha magavana wafanye kazi.
Akiongea jana katika Kongamano la Ugatuzi mjini Homa Bay, Bw Odinga asisitiza kuwa wajibu wa kufuatilia utendakazi wa serikali za kaunti ni wa mabunge ya kaunti wala si Seneti.
“Maseneta hawafai kuwaagiza magavana kufika mbele yao. Ni kupoteza wakati. Mabunge ya kaunti ndiyo yanapaswa kuwaita magavana na kwa hakika wale wanaopaswa kuitwa na seneti ni mawaziri wa kaunti,” akasema.
“Haina haja. Magavana wanapaswa kupewa nafasi ya kushughulikia majukumu yao, sio kutumia muda mwingi Nairobi kuitikia mialiko iliyochochewa kisiasa.”
Bw Odinga pia alitumia jukwaa hilo kuwakashifu wabunge na maseneta kwa kutumia vibaya wajibu wao wa kufuatilia utendakazi wa serikali kwa manufaa yao ya kisiasa na kifedha, akisema hali hiyo inahujumu maendeleo.
“Wakandarasi wanaopoteza zabuni sasa wanatumia madiwani, wabunge na maseneta kuendeleza vita.”
Bw Odinga amewakosoa wabunge na maseneta siku moja baada ya Rais William Ruto kuwashambulia wabunge akidai wao huchukua hongo kutoka kwa wakuu wa mashirika na asasi za serikali ambao huagizwa kufika mbele ya kamati zao kujibu maswali kuhusu masuala mbalimbali.
Huku akiendeleza vita vyake dhidi ya wabunge, Bw Odinga aliwakashifu wabunge kwa kusisitiza kuwa wanapaswa kusimamia fedha za hazina mbalimbali za maendeleo.
Alitoa mfano wa Hazina ya Ustawi wa Maeneo bunge (NG-CDF) inayosimamiwa na wabunge wanaowakilisha maeneobunge, na Hazina ya Kitaifa ya Usawazishaji (NGAAF) inayosimamiwa na Wabunge Wawakilishi wa Kaunti.
“Sio kazi ya wabunge kujenga shule na hospitali. Huu ni wajibu wa magavana. Hazina za NG-CDF na NGAAF zinapasa kuachiwa serikali za kaunti na ziendeshwe pamoja na majukumu mengine yaliyogatuliwa,” akaeleza.
Bw Odinga hakuisaza Idara ya Mahakama akisema kuna madai kwamba baadhi ya watu huwahonga majaji.