Habari

Raila ngangari kucheza 'reggae'

July 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga ametangaza sasa yuko tayari kurejelea shughuli zake za kawaida baada ya kufanyiwa upasuaji katika hospitali moja jijini Dubai.

Bw Odinga alisema Jumatano yu’ buheri wa afya na hivi karibuni, atajibwaga kwenye ulingo wa siasa.

Kupona kwake kunatarajiwa kufanikisha Mpango wa Maridhiano (BBI), almaarufu ‘reggae’ ambao amekuwa akiendeleza na Rais Uhuru Kenyatta kwa lengo la kurekebisha katiba.

Habari za kupona kwake zilitangazwa na bintiye Winnie Odinga, kupitia video aliyoweka kwenye mtandao wa Twitter.

Katika video hiyo, Bw Odinga anaonekana akiwa amesimama wima na kutabasamu, akivalia kinyasa cha rangi ya samawati na fulana ya manjano.

“Ninahisi vyema kuondoka hospitalini na kuvuta hewa safi. Najihisi mwenye nguvu mpya. Hivi karibuni nitaanza kusakata ngoma tena,” Bw Odinga akasema, na kuonyesha mtindo wake wa densi kila anapokuwa jukwaani kuhutubia umati.

Kamati iliyoteuliwa na Rais Kenyatta kuendesha awamu ya pili ya ukusanyaji maoni kutoka kwa umma kuhusu BBI, ilikamilisha kazi yake mwishoni mwa Juni.

Hata hivyo, ilibainika kuwa kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji ingali inasubiri mwaliko wa Rais kumkabidhi ripoti hiyo.

Duru zilisema kuna uwezekano mkubwa Rais alikuwa anasubiri Bw Odinga arejee nchini kwanza. Jumatano, haikufahamika mara moja kama video iliyosambazwa na bintiye Bw Odinga ilikuwa imenaswa humu nchini au ughaibuni.

Bw Odinga aliwashukuru wafuasi wake, hasa vijana kwa kumtakia afueni ya haraka. “Jumbe zenu zimenifanya kupona haraka,” alisema.

Hayo yamejiri wakati ambapo chama chake cha ODM kimetangaza kitatumia Sh1.2 bilioni kwa shughuli mbali mbali mwaka huu wa kifedha.

Kamati ya usimamizi wa chama hicho iliidhinisha bajeti hiyo na kusema baadhi ya pesa hizo zitatumiwa kwa uchaguzi wa mashinani unaotarajiwa mwaka huu iwapo janga la corona litadhibitiwa.

Mwenyekiti wa chama, Bw John Mbadi, alithibitisha kamati hiyo ilikutana wiki iliyopita chini ya uongozi wa Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa ODM.

“Sasa tuna bajeti ya kusimamia shughuli zote za mwaka,” akasema Bw Mbadi.

Bw Odinga amekuwa akiwahakikishia Wakenya kuwa mchakato wa BBI ungali unaendelea na kwamba ‘reggae’ itarejea baada ya janga la corona kukabiliwa.

Kuna uwezekano mabadiliko mengi ya katiba yaliyopendekezwa yatafanywa kupitia bungeni badala ya kuandaa kura ya maamuzi.

Wadadisi wanasema kwamba, mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa na Chama cha Jubilee katika bunge la taifa na seneti yalinuiwa kutengenezea njia mchakato huo.

Katika mabadiliko hayo, wandani wa Naibu Rais William Ruto walipokonywa nyadhifa zao za uongozi bungeni ambazo zimepeanwa kwa wanasiasa wanaoegemea upande wa Rais na Bw Odinga.

Iliaminika kuwa wandani hao wa Dkt Ruto ambao wamekuwa wakipinga mchakato wa BBI wangevuruga juhudi za kupitisha mapendekezo ya ripoti.

Hata hivyo, imefichuka wafuasi hao wa mrengo wa Tangatanga wanatambua upanuzi wa nyadhifa za uongozi huenda ukamnufaisha pia Naibu Rais katika azimio lake la kumrithi Rais Kenyatta ifikapo mwaka wa 2022.

Hii ni kutokana na jinsi itakuwa rahisi kwa mgombeaji urais kushawishi viongozi wengine kuungana naye kama kuna nafasi nyingi za uongozi kugawana.

 

Ripoti za Benson Matheka, Samwel Owino na Valentine Obara