Raila ni Joshua au Judas?
Na BENSON MATHEKA
WAKENYA wameendelea kugawanyika kumhusu Kiongozi wa ODM Raila Odinga, baadhi wakishikilia ndiye atakayesaidia kuleta mabadiliko yenye manufaa kwa nchi, na wengine wakimchukulia kama aliyesaliti msukumo wa utawala bora na demokrasia.
Kabla ya kukubali kufanya kazi na serikali aliyokuwa akikosoa vikali mnamo 2018, Bw Odinga alichukuliwa na mamilioni ya Wakenya kama aliyekuwa na ari na uwezo wa kuwaongoza kutimiza maono ya nchi bora, ndiposa wafuasi wake wakamwita Joshua.
Kulingana na Biblia, Joshua ndiye aliyewaongoza Waisraeli kuingia “nchi ya ahadi” ya Canaan.
Lakini tangu handisheki, wakosoaji walianza kumwita Bw Odinga Judas, ambaye Biblia husimulia kuwa alimsaliti Yesu baada ya kuhongwa.
Wakosoaji wake wanasema kupitia kwa mchakato wa kubadilisha katiba kupitia BBI, Bw amesaliti demokrasia aliyopigania kwa udi na uvumba, na pia wananchi wa kawaida ambao amekuwa mtetezi wao kwa miaka mingi.
Kwa wanaharakati waliowahi kushirikiana naye hasa katika uliokuwa muungano wa NASA na wafuasi wao, Bw Odinga aliwasaliti kwa kuacha ajenda walizokuwa nazo kama upinzani na kuamua kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta.
Akijitetea, Bw Odinga asema kuwa hawangefaulu kwa kukaa katika upinzani, na handisheki yake na Rais Kenyatta ilikuwa ya kuunda daraja ya kuwavukisha Mto Jordan.
Japo wafuasi wake walimuunga mkono wakitarajia kuwa uhusiano wake na Rais Kenyatta ungefanya serikali kuweka mikakati ya kuboresha maisha yao, hali ya maisha ya Wakenya imeendelea kuzorota hata zaidi tangu alipoingia serikalini.
“Aliacha kukosoa serikali na akapotea njia ya kuelekea Canaan akarudi Misri. Alipatiwa kazi na kufurahia uhusiano wake na Rais Kenyatta na kuacha wafuasi wake kwenye jangwa wakibeba mizigo mizito ya madeni ya kigeni, kodi za juu, umaskini na kupoteza matumaini,” alisema mwanaharakati Bonface Mwangi.
Punde tu baada ya kuungana na Rais Kenyatta, Bw Odinga alilaumiwa kwa kupoteza maono aliyokuwa nayo na kuunga mkono serikali kwa masuala aliyokuwa akikosoa.
Hii ilijitokeza wazi aliponyamaza serikali ilipokuwa ikilimbikizia Wakenya madeni, kupitisha sheria za kuwakadamiza na sakata nyingi za ufisadi.
Kwa sasa Bw Odinga anapigia debe BBI akidai kuwa ikipita maisha ya Wakenya yatakuwa mazuri zaidi. Hii ni licha ya ukweli kuwa itaongeza gharama ya kuendesha serikali.
“Niliwaambia tutaenda nchi inayoitwa Canaan. Safari inaendelea. Niliwaambia daraja ni BBI,” alidokeza majuzi.
Dkt Patrick Mbugua wa Chuo Kikuu cha Otago, New Zealand anasema kwamba kinyume na kauli ya Bw Odinga kwamba BBI italeta ustawi Kenya, itaongeza ushindani wa kisiasa na kuzua migawanyiko zaidi.
“BBI sio daraja la ustawi. Lengo lake ni kubuni nyadhifa za uongozi ambazo zitafaidi wanasiasa wachache,” anasema Dkt Mbugua.
Wanaharakati wanasema kwamba kwa wanasiasa watakaonufaika na vitamu katika BBI, wakiwemo vinara wa NASA waliomwita msaliti awali, Bw Odinga atakuwa amewafikisha nchi ya ahadi kwani watakuwa na nafasi bora ya kuingia serikalini.
Ingawa baadhi ya wanaharakati na wataalamu wa katiba wanatofautiana naye kuhusu BBI wakisema Katiba ya 2010 inafaa kutekelezwa kikamilifu kabla ya kuanza kuifanyia marekebisho, kuna wanaohisi kwamba Bw Odinga ametoa Kenya mbali.
“Raila yuko sawa kujifananisha na Joshua kwani ametekeleza jukumu kubwa kupigania siasa za vyama vingi vya kisiasa na utawala wa kidemokrasia nchini,” asema Dkt Bernard Manyibe, mhadhiri kutoka Kenya anayefunza katika Chuo Kikuu cha Langston, Amerika.
Bw Odinga alitupwa kizuizini mara tatu na serikali ya Kanu kwa kupigania demokrasia ya vyama vingi. Ni mmoja wa watetezi maarufu wa utawala bora na haki nchini ambao mchango wao hautasahaulika katika historia ya nchi hii.
Tangu Rais Kenyatta alipoingia madarakani 2013, Bw Odinga alikuwa msitari wa mbele kutetea haki za Wakenya. Alifichua kashfa nyingi za ufisadi ikiwemo ya Eurobond na ya ununuzi wa kiliniki za kuhamishwa ambapo jamaa wa karibu wa Rais Kenyatta walitajwa kuhusika.
Wakati huo alikuwa akiwapa matumaini Wakenya na hakusita kukashifu viongozi na maafisa wa serikali walipokiuka haki za raia nchini, kuendeleza ukabila na kutenga baadhi ya maeneo nchini.
Pia alisimama kidete kutetea idara huru kama vile mahakama.
Wakenya wagawanyika kumhusu Kiongozi wa ODM baadhi wakimwona kama mwokozi, wengine msaliti.