Habari

Raila, viongozi wa kisiasa wajumuika kuifariji familia ya Ken Okoth

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi pamoja na vingozi wengine wa kisiasa wamejiunga na familia ya aliyekuwa mbunge wa Kibra Ken Okoth aliyefariki Ijumaa wiki jana.

Familia ya mwedazake imefanya mkutano Jumatano katika hoteli ya Silver Springs, Nairobi ambapo walitangaza mipango yao ya mwisho.

Akizungumza baada ya mkutano na familia, Bw Odinga amesema kuwa misa za marehemu Okoth zitaanza siku ya Jumatano (leo) ambapo ya kwanza itakuwa katika shule ya Starehe Boys Centre ambako alisomea.

“Baada ya mashauriano na familia, tumefikia uamuzi kwamba misa zitafanyika ikizingatiwa kuwa Gavana wa Bomet Joyce Laboso aliyefariki Jumatatu atazikwa Jumamosi,” amesema Bw Odinga.

Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga (wa pili mbele kushoto) alipotangaza mipango ya mazishi ya Ken Okoth. Picha/ Magdalene Wanja

Kesho Alhamisi misa nyingine itafanyika katika shule ya upili ya Moi, Woodley katika eneobunge la Kibra.

Mwili wa Okoth kisha utasafirishwa hadi eneo la Bondo siku ya Jumamosi.

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja awasili katika mkutano huo. Picha/ Magdalene Wanja

Waliohuhuria mkutano huo ni pamoja na ndugu watatu wa marehemu Okoth.

Bw Odinga amesema kuwa mamake Okoth amekuwa katika ukumbi ila hangeweza kuhudhuria mkutano kwani alikuwa mgonjwa.

Jumamosi, mwili wa Okoth utakabidhiwa familia yake ili kuamua jinsi ya kuuzika.

Misa ya mwisho itafanyika katika eneobunge la Kabondo.

Spika Muturi ambaye alikaa kwa muda wa saa chache amesema kuwa amehudhuria mkutano huo kuwapa pole jamaa wa mwendazake.