Habari

Rais amkemea vikali mbunge

January 29th, 2020 1 min read

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne alimkemea vikali mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, akidai amekuwa akimharibia sifa kwenye vyombo vya habari.

Akiwahutubia wenyeji wa Bahati alipozuru eneo hilo kuzindua miradi kadhaa ya barabara, Rais Kenyatta alisema aliamua mwenyewe kufika katika eneo hilo ili kufahamu ikiwa aliwakosea kwa namna yoyote ile.

“Nimeamua kufika mwenyewe katika eneo hili ili kuwauliza ikiwa yale ambayo mbunge wenu amekuwa akisema dhidi yangu ni ya kweli au la,” akasema.

Bw Ngunjiri amekuwa akimkosoa vikali Rais, akidai amemsaliti na kumtenga Naibu Rais William Ruto licha yao kuchaguliuwa pamoja mnamo 2013 na 2017 kwa tiketi ya Chama cha Jubilee (JP).

Amekuwa akisisitiza kuwa wao wanamtambua Rais na Dkt Ruto, lakini si kinara wa ODM Bw Raila Odinga, ambaye amekuwa karibu na Rais, kufuatia handisheki kati yao mnamo Machi 2018.

Lakini mnamo Jumanne, Rais alisema kuwa mbunge huyo anapaswa kutekeleza majukumu aliyopewa na wapiga kura, mbali si kumwingilia kisiasa.

“Yeye anapaswa kufahamu ninawaongoza zaidi ya Wakenya milioni 40 ambapo nina haki kuchukua hatua yoyote ile ili kuhakikisha utangamano na umoja miongoni mwao,” akasema Bw Kenyatta, akionekana kuitetea handisheki.

Bw Ngunjiri ni miongoni mwa wabunge wa kundi la ‘Tangatanga’ ambalo limekuwa likiishinikiza jamii ya Agikuyu katika maeneo ya Mlima Kenya na Bonde la Ufa kumuunga mkono Dkt Ruto kwenye azma yake ya kuwania urais mnamo 2022.