Habari

Rais Kenyatta afurahia mchango wa vyama vya ushirika katika ustawi wa taifa

July 20th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amepongeza sekta ya vyama vya ushirika nchini kwa wajibu wake wa kuimarisha uchumi wa taifa hili.

Alisema sekta hiyo inamiliki mali ya thamani ya Sh1 trilioni ambayo imekuwa ikipiga jeki uchumi nchini kwa kiwango kikubwa mno.

Rais Kenyatta alisema hayo Jumamosi katika jumba la mikutano ya kimataifa la KICC, Nairobi wakati wa maadhimisho ya 97 ya siku ya Kimataifa ya Ushirika, ambapo alitoa wito wa kuanzishwa kwa mfumo wa pamoja wa kifedha.

Mfumo huo utawezesha vyama vya ushirika kutoa malipo kwa urahisi na kuzindua huduma nyingine kwa wanachama wao.

Kiongozi wa taifa aliongeza kuwa serikali itazindua sera zaidi za kuziba mianya katika shughuli za vyama vya ushirika akisema kuwa sekta hiyo ni mshirika mkubwa katika utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu za serikali.

Rais aliagiza Wizara ya Biashara kurekebisha chama cha Wakulima wa Kahawa Nchini (KPCU) pamoja na Muungano wa Wakulima Nchini (KFA).

Awali, Rais Kenyatta alijiunga na maelfu ya wadau wa sekta ya maziwa wakati wa kufunguliwa upya kwa kiwanda cha utayarishaji maziwa cha New KCC cha Dandora katika kitongoji cha Mowlem, eneobunge la Embakasi Magharibi ambacho kimekarabatiwa.

Ufunguzi wa majumba

Vilevile aliongoza hafla ya ufunguzi rasmi wa wa majumba ya Nachu Plaza na Mwalimu Plaza ambayo yanamilikiwa na vyama vya ushirika.

Alisema kuwa serikali tayari imekamilisha ukarabati kiwanda cha maziwa cha New KCC huko Eldoret na kile cha Sotik.

“Hivi karibuni tutafungua viwanda vya KCC vya Nyahururu na Kiganjo ambavyo vinafanyiwa ukarabati,” akasema Rais Kenyatta huku akishangiliwa na mamia ya wakulima waliohudhuria shughuli hiyo.

Rais Uhuru Kenyatta ajionea baadhi ya bidhaa Julai 20, 2019. Picha/ Hisani

Kiongozi wa taifa alikuwa ameandamana na Waziri wa Biashara, Peter Munya, Gavana wa Nairobi, Mike Sonko miongoni mwa maafisa na viongozi wa tabaka mbalimbali.