Habari

Rais Kenyatta atetea hatua ya kuteua wanajeshi kusimamia asasi za kiraia

October 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ametetea hatua yake ya kuwateua wanajeshi kusimamia asasi za kiraia akisema hatua hiyo imeimarisha utendakazi na kuzima wizi wa mali ya umma katika asasi hizo.

Akiongea Jumanne katika gareji ya Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi katika eneo la Viwanda, alipozindua magari 83 yaliyofanyiwa ukarabati, kiongozi wa taifa alisema ataendelea na mtindo huo – wa kuteua wanajeshi – ili kufanikisha ajenda yake ya maendeleo.

“Wale wanaoongea matope kwa kudai nageuza nchi kuwa ya kijeshi hawaelewi wanayosema. Wanajeshi wetu wameonyesha utendakazi wa haraka na usiojikita katika ufisadi. Na tutaendelea kuwatumia wanajeshi kusimamia taasisi za umma,” akasema Rais Kenyatta.

Akasisitiza: “Siwatumii wanajeshi vibaya katika masuala ya umma. Kile ninafanya ni kutumia Wakenya wa kutegemewa kutimiza ajenda yangu kwa taifa hili. Na KDF ni wenzetu na wao pia ni Wakenya.”

Rais Kenyatta alitoa wito kwa Wakenya wengine wanaohudumu katika sekta mbalimbali za uchumi kuiga mfano wa utendakazi mzuri unaodhihirishwa na wanajeshi, akisema hiyo itahakikisha kuwa Wakenya wanapata huduma kwa wakati.

Aliwasifu wanajeshi kwa kudhihirisha utaalamu wanapotumikia taifa kwa moyo wa kujitolea.

“Ikiwa sote nchini Kenya tungeipenda na kuhudumia taifa letu wanavyofanya wanajeshi wetu, Kenya ingekuwa taifa bora la kupigiwa mfano kote barani Afrika. Sote tunapaswa kujifunza kutoka kwa wanajeshi wetu ambao kando na kulinda taifa hili wameweza kutekeleza kazi ya ujenzi na ukarabati wa miundo msingi muhimu nchini,” akasema Rais Kenyatta.

Kiongozi wa taifa aliipongeza NMS chini ya usimamizi wa Meja Jenerali Mohammed Badi kwa utendakazi mzuri ambao umebadilisha sura ya Nairobi tangu ilipewa wajibu wa kusimamia majukumu manne ya kaunti ya Nairobi.

Magari 83 ambayo Rais Kenyatta alizindua yalifanyiwa ukarabati kwa kipindi cha miezi miwili pekee kwa gharama ya Sh22 milioni. Hii ni baada ya gareji hiyo kuwekwa chini ya usimamizi wa NMS.

Rais Kenyatta pia alitoa mfano wa miradi mbalimbali ya miundomsingi ambayo yamekarabatiwa na wanajeshi, ikiwemo njia za reli na bandari ya Kisumu na meli ambayo huhudumu katika Ziwa Victoria.

Mwezi jana, Mbunge wa Kandara Alice Wahome aliwasilisha kesi mahakamani kupinga hatua ya Rais Kenyatta kumruhusu Meja Badi kuhudhuria na kushiriki shughuli za baraza la mawaziri, akisema hatua hiyo ni kinyume na sheria.

Maseneta nao wamepinga hatua ya kiongozi wa taifa kuweka usimamizi wa Kiwanda cha Nyama Nchini (KMC) chini ya usimamizi wa KDF wakisema bunge lilipasa kushirikishwa katika mpango huo. Hii ni kwa sababu kiwanda hicho ni shirika la serikali lililobuniwa kupitia sheria iliyotungwa na bunge.