Rais Paul Biya, 92, kusaka uongozi kwa muhula wa nane
RAIS wa Cameroon Paul Biya, mwenye umri wa miaka 92, ametangaza kuwa atawania urais tena hapo Oktoba 12 mwaka huu akilenga kuongoza kwa muhula wa nane.
Biya, ambaye ndiye rais mwenye umri mkubwa zaidi duniani kwa sasa, alitangaza hayo kupitia taarifa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X, aliyoiandika kwa lugha za Kifaransa na Kiingereza.
“Nitashiriki katika kinyang’anyiro cha urais,” aliandika na kuongeza: “Nawahakikishia kwamba kujitolea kwangu kuwatumikia kunaafiki dharura zinazosababishwa na changamoto zinazotukabili.”
Biya aliingia mamlakani mwaka 1982 baada ya kujiuzulu kwa mtangulizi wake Ahmadou Ahidjo.
Hali yake ya afya imezua gumzo na wasiwasi mara kadhaa nchini humo, haswa mwaka jana alipokosa kuonekana hadharani kwa siku 42.