Rais Ruto aachia eneo la Magharibi miradi ya mabilioni
ZIARA ya siku nne ya Rais William Ruto imeacha eneo la Magharibi na miradi ya mabilioni ya pesa, hatua hiyo ikihusishwa na siasa za uchaguzi mkuu wa 2027.
Rais Ruto alizindua miradi mbalimbali ya maendeleo na anaonekana kulenga kuteka eneo hilo kisiasa. Magharibi imekuwa ngome ya kisiasa ya marehemu Raila Odinga ambaye alikuwa akishinda kura za eneo hilo kila uchaguzi.
“Tunawekeza Sh21 bilioni kwenye miradi ya kuinua Kaunti ya Kakamega na hii inaonyesha kuwa tunamakinika maendeleo sawa kwenye maeneo yote,” akasema Rais Ruto akiwahutubia viongozi wa eneo hilo katika Ikulu ndogo ya Kakamega.
Kati ya miradi hiyo ni Sh14 bilioni za mradi wa Nyumba za gharama nafuu, Sh2.5 bilioni za kujenga masoko na Sh2 bilioni za kujenga vyumba vya malazi kwa wanafunzi katika vyuo vikuu na taasisi za masomo.
Pia rais alitangaza ujenzi wa kiwanda cha kuandaa dhahabu kwa kima cha Sh1.5 bilioni eneo la Ikolomani.
“Tumeanzisha ujenzi wa kilomita 230 za barabara katika kaunti na pia tumetenga Sh2.6 bilioni kuunganisha umeme katika nyumba 34,000,” akasema Rais Ruto.
Pia kiongozi wa nchi alitangaza kuwa serikali yake inaendelea kuzungumza na Benki ya AfDB kupokea mkopo wa Sh600 milioni. Ikifaulu, basi mgao ambao umetengewa umeme utakuwa Sh3.2 bilioni katika Kaunti ya Kakamega.
Kwenye ziara hiyo, Rais aliandamana na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla, Gavana Ferndandes Barasa, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli, makatibu, wabunge, madiwani miongoni mwa viongozi wengine.
Pia Rais aliahidi kuwa analenga kuhakikisha kuwa ujenzi wa uga wa Bukhungu na Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kakamega unakamilishwa.
“Nimekubaliana na Gavana Fernandes Barasa kwamba serikali ya kitaifa itaendeleza ujenzi wa hospitali hii ili ikamilike haraka. Tumetenga Sh1.4 bilioni kumaliza ujenzi wa Bukhungu kisha Sh1 bilioni kwa hospitali ya mafunzo na rufaa, hizi mbili zikiwa miradi muhimu ya michezo na afya,” akasema Rais Ruto.
Hapo jana, Rais alifafanua kuwa kwa ujenzi wa hospitali hiyo utakamilika ndani ya miezi 10.
“Nimemwambia Gavana Fernandes Barasa kuwa hospitali hii ni kubwa na anastahili kuniachia niikamilishe,” akasema Rais Ruto.
Hata hivyo, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alikashifu baadhi ya miradi akisema ni kama rais anafanyia tu eneo hilo majaribio kupima uungwaji mkono wake.
“Baadhi ya miradi kama Barabara ya Malava-Samitsi-Navakholo imezinduliwa mara nne na mtu mmoja. Hana aibu akizundua mradi moja zaidi ya mara nne?” akauliza Dkt Khalwale.
Seneta huyo alidai kuwa Rais anapoenda Mlima Kenya anaacha miradi muhimu na anapofanya ziara Nyanza anazindua miradi ya mabilioni.
“Akija hapa Magharibi anahudhuria ibada ya kanisa na kuzindua miradi zaidi ya mara moja,” akasema Dkt Khalwale.