Habari

Rais Ruto apeleka minofu Kakamega

Na SHABAN MAKOKHA October 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amesisitiza azma ya serikali yake ya kuharakisha maendeleo katika kila eneo la Kenya, akikanusha madai kwamba baadhi ya sehemu zimeachwa nyuma.

Akizungumza Alhamisi alipoanza ziara ya siku nne ya maendeleo Magharibi mwa Kenya, Rais alisema hakuna eneo lolote litakalobaki nje ya ajenda ya serikali ya ukuaji wa haki.

“Uamuzi wangu ni kuhakikisha hakuna eneo linalobaki nyuma katika mpango wa maendeleo wa serikali. Ndio maana ninatoka sehemu moja hadi nyingine ili kila Mkenya apate kipande cha raslimali ya taifa,” alisema.

Katika awamu ya kwanza ya ziara yake, Rais Ruto alizindua rasmi Hospitali ya Level 4 Butere na kuzindua ujenzi wa barabara tatu katika Kaunti za Malava, Lugari na Shinyalu.

Alitangaza kuwa serikali imetenga Sh2.5 bilioni kwa barabara za Kakamega, Sh2.2 bilioni kuunganisha familia 340,000 na umeme, na Sh1 bilioni kukamilisha Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kakamega.

Hospitali ya Level 4 Butere, ambayo ilizinduliwa awali na Gavana wa zamani Wycliffe Oparanya mwaka 2022, itapatiwa vifaa vya kisasa vya thamani ya Sh150 milioni.

Rais pia alishambulia vikali viongozi wa upinzani, akiwashutumu kwa kuunda propaganda za kuvuruga miradi ya serikali.

Aliwataja kama watu wasiokuwa na mpango wowote wa taifa na kudai wanataka kudhoofisha ajenda yake ya maendeleo kabla ya uchaguzi wa 2027.

Alilenga aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua, akisema amejawa na hasira na haafai kuongoza.

“Kazi yake kuu ni kusambaza chuki, kugawanya Wakenya kwa makabila na kutukana viongozi. Je, anadhani kwa kupiga kelele ‘Wantam na Kasongo atanishinda 2027?” alihoji.

Rais alisisitiza kuwa kipaumbele chake kikuu ni utoaji wa huduma na miradi ya maendeleo.

“Kwa sasa, niko makini kutoa miradi kwa Wakenya wote. Hii ndiyo ajenda yangu kuu. Nitawaonyesha siasa ni nini 2027 kwa sababu mtu pekee aliyenitisha alikuwa ndugu yangu marehemu, Raila Odinga. Wengine ni rahisi kushinda,” alisema.

Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa alipongeza jitihada za Rais za kufikisha vifaa katika hospitali ya Butere, akisema hatua hiyo itaimarisha huduma za afya sehemu ya chini ya Kakamega.