Habari

Rais Ruto azindua mradi wa barabara kuu ya Nairobi-Nakuru-Mau Summit

Na WINNIE ONYANDO November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto Novemba 28, 2025 alisema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Nairobi–Nakuru–Mau Summit utagharimu Sh170 bilioni.

Kulingana na kiongozi huyo wa nchi, hatua hiyo imewezekana tu kupitia ushirikiano.

“Ni uwekezaji wa zaidi ya Sh170 bilioni. Ishara kamili kuwa ushirikiano hasa na sekta ya kibinafsi una umuhimu,” Rais alitangaza wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika Kaunti ya Kiambu.

Dkt Ruto alirejelea mradi huo kama “mapambazuko ya enzi mpya,” akisema, “Barabara kuu moja inaweza kumeza karibu nusu ya bajeti yetu yote ya maendeleo ya mwaka,”

“Kama tungesubiri bajeti ya taifa kutoa rasilimali za mradi huu, tungesubiri maisha yetu yote. Ikiwa tungekopa, tungeongeza madeni yetu na kuwafinyilia watoto wetu na vizazi vijavyo,” alisema.

Barabara kuu zilizoboreshwa zitakuwa na sehemu za kuegesha lori, madaraja, mifereji ya maji iliyoimarishwa na miundombinu za kisasa hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari na pia kupunguza ajali barabarani.