Refarenda yaja – Uhuru
JUMA NAMLOLA na CECIL ODONGO
RAIS Uhuru Kenyatta sasa ametoa kauli rasmi kwamba, huenda Wakenya wakashiriki kura ya maamuzi kuhusu wanayotaka yarekebishwe kwenye Katiba ambayo inatimiza miaka kumi leo Alhamisi.
Kwenye hotuba yake ya 11 tangu kutangazwa kwa kisa cha kwanza cha maambukizi ya Covid-19, Rais alisema wakati wa marekebisho ya Katiba umefika.
“Walioandika Katiba hii walisema kwamba, kuna nafasi ya mabadiliko mbeleni. Wakati wa kuibadilisha miaka 10 baadaye umefika. Jinsi nilivyosema wakati wa sherehe za Madaraka, lazima Katiba yetu iwiane na matukio ya kisasa,” akasema.
Marekebisho hayo yataongozwa na mapendekezo yaliyo kwenye ripoti ya mwisho ya jopo la Upatanishi (BBI), iliyosimamiwa na Seneta wa Garissa, Mohamed Yusuf Haji.
Akiwa Ikulu ya Nairobi jana, Rais alisema katika wiki tatu zijazo, atafanya mkutano mkuu utakaowaleta pamoja viongozi wa tabaka mbalimbali ili kujadiliana kuhusu Kenya atakayoachia vizazi vijavyo.
“Baada ya wiki tatu, tutakuwa na mkutano mkubwa wa wadau wote – serikali za kaunti, serikali kuu, makanisa, maimamu, wafanyibiashara, mashirika ya kijamii na wale wote ambao wana nia njema kwa taifa la Kenya. Tutajadiliana tupange na kujua ni kwa njia gani tutapeleka mbele taifa letu,” akasema.Utafiti uliofanywa na shirika la Trends and Insight Africa (TIFA) mwishoni mwa mwaka jana, ulionyesha kuwa Wakenya wengi hawafahamu yaliyomo kwenye ripoti hiyo. Wale wanaoyafahamu, wanataka yatekelezwe kupitia kura ya maamuzi, badala ya Bunge.
Wakati huo, asilimia 69 ya Wakenya, wengi wao wakiwa wanawake walio na umri wa chini ya miaka 24, walisema hawafahamu inavyosema ripoti hiyo.
“Kuna wanawake wengi wasiofahamu yaliyomo kwenye ripoti ya BBI kuliko wanaume. Wale walio na umri wa kati ya miaka 18 na 24 ndio wengi ikilinganishwa na wale walio na umri wa miaka 25 na zaidi,” TIFA ikasema kwenye utafiti wake.
Ripoti hiyo ilizinduliwa katika ukumbi wa Bomas of Kenya mnamo Novemba 27, 2019, ambapo serikali iliahidi kuchapisha nakala za kutosha na kuzisambaza mashinani.
Punde baada ya uzinduzi huo, viongozi wanaomuunga Naibu Rais William Ruto, wanaotambuliwa kama kundi la ‘Tangatanga’, walisisitiza kukataa marekebisho yoyote ambayo lengo ni kuunda nyadhifa za uongozi kunufaisha watu wachache.
Kauli yao ilitokana na mapendekezo kwamba, serikali ipanuliwe chini ya muafaka wa ‘handisheki’ ili viongozi wanaoshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Urais wapate kazi serikalini au katika afisi ya Upinzani inayotambuliwa na sheria.
Dkt Ruto alinukuliwa mara kadhaa na akatumia mtandao wake wa Twitter kusisitiza kutokubali marekebisho hayo, aliyoamini yalilenga kumtengezea nafasi ya uongozi kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga.