Ripoti: Ugatuzi sasa ni mishahara tu na ufisadi, pesa hazitengewi maendeleo
MIAKA miwili baada ya kukumbatiwa kwa serikali za ugatuzi, kaunti zinaonekana zimegeuzwa maeneo ya ajira na ufisadi huku malengo ya maendeleo yakionekana kutelekezwa kwa sababu miradi imetengewa rasilimali chache.
Imebainika kaunti nyingi hutumia mabilioni ya pesa kulipa mishahara, vibarua, marupurupu na shughuli nyingi, pesa ambazo zingezisaidia kupiga hatua iwapo zingetumika kwa miradi ya maendeleo.
Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Mdhibiti wa Bajeti (COB) na Tume ya Kutathmini Misharahara ya Watumishi wa Umma (SRC), zinaonyesha kuwa kaunti kadhaa hutenga kati ya asilimia 60 hadi 70 kwa miradi ya maendeleo.
Kiasi hicho kinazidi kile cha asilimia 35 ambacho kimenakiliwa kwenye Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Pesa za Umma mnamo 2012.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uhasibu kwenye Bunge la Seneti Moses Kajwang’ amesema mtindo huo ni hatari na hauwezi kuvumiliwa.
“Kaunti ambazo zinaelekeza pesa nyingi kwenye mishahara huwa hazina pesa za maendeleo na huu ni mtindo hatari. Magavana wanastahili kutoa kipaumbele kwa maendeleo badala ya ajira,” akasema Bw Kajwang’.
Nakuru ni kati ya kaunti ambazo zinaelekeza pesa nyingi kwenye miradi ya maendeleo. Katika bajeti yake ya 2025/26 ya Sh20.7 bilioni, Sh14 bilioni zitaelekezwa kulipa mishahara na mahitaji mengine ya afisi.
Ni Sh6 bilioni pekee ambazo zitasalia kwa miradi ya maendeleo, hii ikiwa na maana kuwa asilimia 66 hutumika kulipa mishahara. Kaunti hiyo sasa inalenga kujikusanyia mapato yake hadi ifike Sh4.6 bilioni kwa mujibu wa stakabadhi za bajeti.
Kaunti ambazo mgao mkubwa wa bajeti huelekezwa katika kulipa mishahara ni Nyeri, Nairobi, Elgeyo Marakwet, Laikipia zote kwa asilimia 55 kisha Machakos na Nyamira kwa asilimia 55.2.
Taita Taveta (asilimia 53.2), Tharaka Nithi (asilimia 52.3), Murang’a (asilimia 54) na Homa Bay (asilimia 53) pia zinaelekeza pesa nyingi kulipa mishahara. Kisumu, Kericho na Bomet pia ziko kwenye orodha hiyo.
Kaunti tano ambazo zinatumia pesa za chini katika ulipaji mishahara ni Kilifi (asilimia 26.2), Tana River (asilimia 29.4), Busia ( asilimia 31.0), Narok (asilimia 32) na Kwale.