Habari

Ripoti ya BBI tayari kupakuliwa

November 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) itawasilishwa rasmi kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika Ikulu ya Nairobi Jumanne wiki ijayo.

Kwenye kikao cha Ijumaa na wanahabari katika hoteli ya The Stanley, Nairobi, mwenyekiti wake Yusuf Haji, alisema wanachama alisema walikamilisha kuandaa ripoti hiyo mnamo Oktoba 23 na wamekuwa wakisubiri idhini kutoka Ikulu ili waiwasilishe rasmi.

“Ni furaha yetu kujulisha umma kwamba Ikulu imetuhakikishia kwamba tutapata nafasi ya kuwasilisha ripoti hii rasmi kwa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga mnamo Jumanne, Novemba 26 mwendo wa saa tatu asubuhi,” akasema.

Na saa chache baada ya Bw Haji ambaye ni Seneta wa Garissa kutoa tangazo hilo, Rais Kenyatta amewataja wale ambao wamekuwa wakipinga ripoti hiyo hata kabla ya kutolewa kwake kama “wajinga.”

“Kuna hawa watu wanaosema hawataki BBI ilhali hawajaona yaliyomo ndani yake. Hawa ni wajinga kwa sababu wanapinga kile ambacho hawajaona,” akasema kiongozi wa nchi alipoongoza hafla ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Kibabii, Kaunti ya Bungoma.

Akaongeza: “Tunawapeleka watu shule ili waweze kufundishwa kusoma. Kwa hivyo, tunapaswa kutumia muda wetu, tuisome pamoja na kuibuka na mambo mazuri ambayo yanaweza kuboresha nchi hii, ambayo yanaweza kufanya taasisi zetu kushirikisha wote na kuleta umoja nchini.”

Rais Kenyatta alithibitisha kuwa ataipokea ripoti hiyo Jumanne alivyotangaza Bw Haji.

“Nimewaambia kuwa wako huru kuileta Jumanne. Na nawahakikishia kuwa baada ya kuipokea binafsi nitaisoma kabla kuitoa kwa Wakenya wote,” akasema huku akiwataka wanasiasa kukoma kuingiza siasa katika ripoti hiyo.

Tangu jopokazi hilo kukamilisha kuandaa ripoti hiyo Oktoba wabunge kutoka mrengu wa Tangatanga wamekuwa wakitisha kuipinga endapo itapendekeza mageuzi ya Katiba ili kubuniwa kwa nafasi zaidi za uongozi.

Wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto viongozi hao wametoa ahadi kupinga ripoti hiyo ikiwa itapendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa uongozi wa ubunge kwa kubuniwa kwa nyadhifa za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili.

Kwa upande mwingine, wanasiasa wanaoegemea mrengo unaounga mkono muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakiipigia debe ripoti hiyo, wakisema imesheheni “mambo mazuri ya kuboresha nchi katika nyanja zote.”

Bw Haji amepuuzilia mbali yale aliyoyataja kama uvumi kuhusu yaliyomo katika ripoti hiyo, huku akivitaka vyombo vya habari kukoma kusambaza habari kama hizo alizozitaja kama ‘feki’.

“Ripoti kama hizi za kupotosha zinalenga kuwakanganya na kuleta miganyiko miongoni mwa Wakenya hasa zinaposambazwa katika mitandao ya kijamii. Huu ni wakati ambapo kuna muafaka kuhusu haja ya kuwepo kwa uwiano na utangamano wa kitaifa,” akasema huku akiwa ameandamana na baadhi ya wanachama 14 wa jopokazi hilo.

Akaongeza: “Tunawaomba wanahabari na umma kwa jumla kuwasiliana nasi ili wathibitishe ripoti, taarifa na barua mbalimbali yanayodaiwa kutoka kwa jopokazi la BBI.”

Mwenyekiti huyo alisema walipokea maoni na mapendekezo kutoka kwa zaidi ya Wakenya 7,000 kutoka tabaka mbalimbali katika vikao walivyoandaa katika kaunti zote 47.

“Jopokazi hili pia lilipokea maoni kutoka watu 123 waliowakilisha asasi mbalimbali na zaidi ya viongozi 400 waliochaguliwa; wa sasa na zamani. Aidha, tulipokea memoranda 755 katika vikao hivyo,” Bw Haji akasema huku akiwashukuru wote waliofika mbele ya wanachama wake.

Jopokazi hilo liliundwa baada ya muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga mnamo Machi 9, 2018, kupendekeza njia za kupata suluhu kwa mambo mbalimbali ambayo huleta machafuko kila baada ya uchaguzi mkuu.

Baadhi ya masuala ambayo lilishughulikia ni pamoja na ukabila, baadhi ya watu kuhisi kutengwa serikalini, njia za kukomesha ufisadi, namna ya kuimarisha mfumo wa uchaguzi, kuimarisha ugatuzi, usawa, miongoni mwa mengine.

Wanachama wa jopokazi hili ni; Adams Oloo (Naibu mwenyekiti), Agnes Kavindu, Florence Omose, Saeed Mwanguni, Mzee James Matundura, Meja John Seii, Askofu Lawi Imathiu na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Samburu Bi Maison Leshomo. Wengine ni; Morompi Ole Ronkai, Askofu Peter Njenga, Mbunge Rose Moseu na Askofu Mkuu mstaafu Zacheaus Okoth.

Na makatibu wenza wake ni Bolozi Matin Kimani na Wakili Paul Mwangi.