Habari

Ripoti ya KNBS onyesha kupungua kwa ajira katika sekta ya ujenzi

Na PETER MBURU May 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI za ujenzi za kibinafsi zilipunguza wafanyakazi 2,900 mwaka jana huku sekta hiyo ikidorora kwa asilimia 0.7, kutokana na wawekezaji kusita kuwekeza kutokana na kupanda kwa gharama za vifaa na kupungua kwa mikopo kutoka kwa benki.

Kampuni hizo zilikuwa na wafanyakazi 223,400 kutoka watu 226,300 mwaka wa 2023, huku serikali ikiongeza ajira kwa watu 200 katika sekta ya ujenzi na kufikia watu 9,900, kulingana na Ripoti ya Uchunguzi wa Kiuchumi ya 2024.

“Sekta ya ujenzi ilipungua kwa asilimia 0.7 mwaka wa 2024 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3 ulioshuhudiwa mwaka wa 2023. Kulikuwa na kasi ndogo katika miradi ya miundombinu ya umma na maendeleo ya sekta  ya kibinafsi, hali iliyoashiria kipindi cha marekebisho kwa sekta hiyo,” ilisema ripoti ya Shirika la  Kitaifa la Takwimu Kenya (KNBS).

KNBS ilitaja vikwazo vya kimfumo kama vile ukosefu wa upatikanaji wa  mikopo nafuu na kupungua kwa imani ya wawekezaji kama sababu kuu za matatizo ya sekta hiyo mwaka jana.

Ripoti hiyo inayoonyesha kupungua kwa ajira katika sekta ya ujenzi mwaka wa 2024 inazua maswali kuhusu mahali zilipo ajira elfu nyingi ambazo serikali imekuwa ikidai imeundwa kupitia mpango wa nyumba za bei nafuu tangu mwaka wa 2023.

Mwezi Desemba mwaka jana, Rais William Ruto alisema kuwa ajira 200,000 zimeundwa kupitia mpango wa nyumba za bei nafuu.

“Nguzo ya kimkakati ya nyumba za bei nafuu katika Ajenda ya Mageuzi ya Kiuchumi Kutoka Chini Kuenda Juu tayari imeunda ajira 200,000 na maelfu ya fursa zisizo za moja kwa moja katika mfumo wa ujenzi na maendeleo,” alisema Rais Ruto wakati wa sherehe za Jamhuri Day.

Wakati wa sherehe za Siku ya Wafanyakazi wiki iliyopita, Rais alisema idadi ya ajira kupitia mpango huo iliongezeka hadi kufikia 250,000.

“Kufikia mwisho wa Aprili, tayari tulikuwa tumeunda zaidi ya ajira 250,000 zinazohusisha usanifu majengo, uhandisi, upangaji miji, uashi, useremala, uwekaji mabomba, na kazi za umeme, na kuinua uchumi wa maeneo ya ndani,” alisema.

Haijakuwa wazi ni kwa nini licha ya madai ya serikali kuwa imeunda maelfu ya ajira kupitia mpango huo, sekta ya ujenzi inapoteza ajira.

Katibu wa Wizara ya Makazi Charles Hinga, alisema jana kuwa “takwimu zetu zinatokana na kazi halisi inayofanyika. Tuna zaidi ya nyumba 130,000 ambazo zinajengwa.”

Hadi kufikia Februari, Hazina ya Kitaifa ilikuwa imesema kuwa nyumba 124,000 zilikuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Katika Ripoti ya Uchunguzi wa Kiuchumi, KNBS ilitaja sababu kama ongezeko la bei ya vifaa vya ujenzi kwa asilimia 2.83 ikilinganishwa na asilimia 2.3 mwaka wa 2023, kama miongoni mwa vichocheo vya kupungua kwa ajira katika sekta ya ujenzi.

Sababu hizo zilipelekea kupungua kwa shughuli katika sekta hiyo, huku matumizi ya saruji yakishuka kwa asilimia 7.2 na kufikia tani milioni 8.537 mwaka wa 2024.

Benki za kibiashara pia zilipunguza mikopo kwa sekta ya ujenzi kutoka Sh602.7 bilioni mwaka wa 2023 hadi Sh528 bilioni.

“Ajira katika sekta ya kibinafsi ya ujenzi ilionyesha mwelekeo wa kushuka, ikipungua kutoka wafanyakazi 226,300 mwaka wa 2023 hadi 223,400 mwaka wa 2024. Ajira ya umma katika sekta hiyo iliongezeka kutoka wafanyakazi 9,700 mwaka wa 2023 hadi 9,900 mwaka wa 2024,” ilisema ripoti hiyo ya Uchunguzi wa Kiuchumi.