Habari

Ruku: Rais Ruto ni mchapakazi, watumishi wa umma wamuige kutoa huduma kwa Wakenya

Na GEORGE MUNENE April 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku amewaonya watumishi wa umma wazembe kuwa watachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kuachishwa kazi.

Bw Ruku alisema Rais William Ruto ni mchapakazi na watumishi wote wa umma wanastahili kumuiga kwa kutoa huduma bora kwa Wakenya.

“Watumishi wa umma ambao wanafeli kutoa huduma watakabiliwa vikali kisheria. Rais amenipa jukumu la kuhakikisha Wakenya wanahudumiwa vyema,” akasema Bw Ruku.

Kiongozi huyo ambaye aliapishwa wiki jana, alisisitiza kuwa lazima Wakenya waunge mkono utawala uliopo ndipo serikali nayo iwahudumie kwa urahisi mno.

Alikuwa akiongea katika Kanisa la Baptist la Itugururu eneobunge la Chuka Igambangómbe Kaunti ya Tharaka-Nithi. Waziri huyo alikuwa amehudhuria hafla ya kutawazwa kwa mhubiri Anderson Mwiathi.

Kabla ya kuteuliwa waziri, Bw Ruku alikuwa mbunge wa Mbeere Kaskazini na alisema kuwa atamakinika kuunga juhudi zote za serikali kuimarisha utendakazi wake na kubadilisha maisha ya raia.

“Hii nchi ilikuwa katika hali mbaya kiuchumi Rais Ruto alipochukua hatamu za uongozi. Hata hivyo, miradi ambayo ilikwama sasa inaendelea na rais na naibu wake wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa kuna maendeleo pembe zote za nchi,” akasema Bw Ruku.

Alitaja babarabara ya Itugururu-Mate kwenye eneobunge la Chuka Igambangómbe kati ya miradi iliyokwama na sasa inaendelea na akaahidi kuwa miradi mingine inayoendelea pia itakamilishwa kwa wakati.

Kwenye wizara yake, Bw Ruku alisema atashirikiana na idara zote za serikali kutekeleza mageuzi yanayolenga kuboresha utendakazi wa utawala wa sasa.

Aliwahakishia Wakenya kuwa watahudumiwa bila ubaguzi wowote akiahidi binafsi atamakinika kuhakikisha idara zote zinawawajibikia majukumu yao na kufuata sheria.

“Kama serikali inafanya kazi basi njia bora ni kuirejesha mamlakani mnamo 2027. Tunastahili kumakinika kumaliza miradi na Wakenya wamchague rais kutokana na utendakazi wake,” akasema.

Akionekana kuwalenga wapinzani wa Rais Ruto, waziri huyo aliwataka Wakenya wawapuuze kwa sababu hawana suluhu kutokana na masuala wanayoyaibua.

“Hata wakikosoa serikali, hawapendekezi suluhu wala hawana mamlaka ya kuyatekeleza yale wanayoyasema,” akasema.

Kati ya miradi ya serikali aliyowataka Wakenya wajisajili ni Bima ya Afya ya Kijamii (SHA), akisema bima hiyo sasa inafanya kazi na wagonjwa waliojisajili sasa wanalipiwa gharama ya matibabu.

Mbunge wa Chuka Igambangómbe Patrick Munene alimshukuru Rais Ruto kwa kumteua Bw Ruku waziri akisema kuwa anatosha kuchapa kazi kwenye wadhifa huo.

“Ni rahisi kumfikia Ruku na kuzungumza naye licha ya hadhi yake serikalini,” akasema Bw Munene.

Mbunge huyo alisema Mlima Kenya Mashariki unaunga mkono utawala wa Kenya Kwanza kutokana na miradi iliyoanzishwa na inayoendelea kutekelezwa.

Mkuu wa Kanisa la Baptist ukanda wa Mlima Kenya Albert Gitonga alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya kanisa na serikali. Alisema kwa kuwa kanisa linawaombe viongozi, lazima liwaunge mkono kwenye utendakazi wao.