Habari

Ruku: Tutaongeza wafanyakazi mishahara, tuwafunze kutumia AI wapate motisha kazini

Na CECIL ODONGO September 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku amesema kuwa serikali itaendelea kuwatia motisha wafanyakazi wake kupitia nyongeza ya mshahara na mafunzo kuhusu teknolojia ya Akiliunde (AI) ili kuimarisha utoaji wa huduma.

Bw Ruku alikiri kuwa kuna mwanya mkubwa katika ulipaji mshahara miongoni wa watumishi wa umma na akasema juhudi zinaendelea ili kuhakikisha kuna usawa ndipo wafanyakazi wengine wasihisi wamebaguliwa.

“Serikali inamakinikia usawazishaji wa mshahara na mapato mengine kwa watumishi wa umma kama sehemu ya mbinu zake za kuwatia motisha. Sote tunamakinika kuhakikisha kuna usawa katika ulipaji wa mishahara miongoni mwa wafanyakazi wa serikali ndipo kuwe na huduma bora,” akasema Bw Ruku.

“Kuna malalamishi ambayo yameibuliwa katika ulipaji wa mshahara lakini tunamakinika kuhakikisha kuwa kuna usawa ili kila moja afurahi kazini,” akaongeza.

Alikuwa akiongea wakati wa  kufunga Makala ya 44 ya Michezo ya Watumishi wa Umma uwanja wa Moi Kaunti ya Embu.

Waziri huyo aliwasifu watumishi wa umma kutokana na kujituma kwao na kuzingatia maadili wanapowahudumia Wakenya.

“Mnafanya kazi nzuri na kwa ujasiri mkubwa nasema watumishi wa umma wa Kenya ndio bora zaidi Afrika,” akasema.

Bw Ruko pia alipigia upato matumizi ya teknolojia na mageuzi yanayoendelezwa na Wizara ya Teknolojia na Mawasiliano kuhakikisha sekta ya utumishi wa umma ina usasa.

Alisema matumizi ya AI na zana zake kutasaidia kuimarisha utoaji wa huduma ndipo Wakenya wasitatizike.