Habari

Ruto aagiza waporaji na wachomaji wa biashara wapigwe risasi mguuni

Na FATUMA BARIKI July 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto ametaka waporaji na wachomaji biashara za watu washughulikiwe kwa kupigwa risasi mguuni ila polisi wahakikishe hawawatoi uhai.

Akizungumza Jumatano, Julai 9, 2025 katika eneo la Kilimani, Nairobi, wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, Rais Ruto alisema serikali iko tayari kufanya chochote kinachohitajika kulinda mali na biashara za Wakenya.

“Mtu ambaye anaenda kuchoma biashara ya mtu mwingine. Mtu ambaye anachukua moto anaenda kuchoma biashara ya mtu, anaenda kuchoma mali ya watu wengine. Mtu kama huyo apigwe risasi kwa mguu aende hospitali akienda kortini. Wasimuue lakini wampige hii miguu ivunjike ndio aende hospitali ndio aende kortini,” akasema Dkt Ruto.

Alisema askari hawafai kupiga wananchi risasi kuwaua, “lakini mhalifu, mtu ambaye amekwenda kuvunja biashara ya mtu mwingine, ashughulikiwe.”

Bw Ruto alishangaa kwa nini malalamishi na maandamano yamelipuka wakati wa utawala wake akisema Rais Moi, Rais Kibaki na Rais Kenyatta walikabiliwa na ukosefu wa ajira kama utawala wake lakini hawakuandamwa na maandamano kama yanayoshuhudiwa kwa sasa.

Rais alizungumza siku mbili baada ya maandamano ya Saba Saba yaliyoshuhudia watu 31 wakiuawa huku 107 wakijeruhiwa wakati polisi walipokabiliana na makundi ya vijana.

Wengi wa waandamanaji walikuwa wakitoa kauli-mbiu za “Ruto Must Go” yaani “Ruto aondoke mamlakani” huku wengine wakisema anafaa kuhudumu muhula mmoja pekee, yaani “WanTam”.