Habari

Ruto aahidi kuondoa viza Afrika akitwaa usukani Comesa

Na LUKE ANAMI October 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto alitwaa uenyekiti wa Jumuiya ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Kusini (COMESA) na akaahidi kuongoza juhudi za kuondoa masharti ya viza kwa Waafrika na kutatua mizozo inayokumba bara.

Rais Ruto alichukua hatamu kutoka kwa Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, wakati wa Kikao cha 24 cha Wakuu wa Nchi wa COMESA kilichofanyika jijini Nairobi, Alhamisi.

Kikao hicho cha COMESA kinachojumuisha wakuu wa nchi kutoka mataifa 21 wanachama ndicho chombo cha juu zaidi cha kufanya maamuzi katika jumuiya hiyo.

Rais Ruto alisema kuwa juhudi za kuunganisha Afrika haziwezi tu kuishia kwa mikataba ya kibiashara na masoko ya pamoja, bali ni lazima ziendelee hadi kufanikisha uhuru wa watu kusafiri, kufanya kazi, na kuwekeza kokote barani.