Habari

Ruto aahidi kufuta ada ya kitambulisho iliyowekwa na Kindiki alipokuwa waziri

Na KEVIN CHERUIYOT March 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto Alhamisi alitangaza kuwa Wakenya sasa watapewa vitambulisho bila kuhitajika kulipa Sh300.

Kauli yake katika eneobunge la Kibra ilitokana na kilio cha jamii ya Wanubi kwamba wamekuwa wakihangaishwa wanaposaka stakabadhi hiyo muhimu.

“Nimesema ubaguzi katika kutoa kwa kitambulisho unafaa kuisha,” akasema Rais.

Rais pia alifutilia mbali ada ya Sh1,000 ili kupata kitambulisho kipya ikiwa mtu amepoteza chake bila kusumbuliwa.

Alimtaka Bw Orero ahakikishe kuwa ubaguzi ambao umekuwa ukishuhudiwa miaka nenda miaka rudi jamii hiyo inaposaka kitambulisho, unamalizwa.

Awali Orero alikuwa ameitaka serikali itambue Wanubi kama mojawapo ya makabila nchini kwa kuchapisha hatua hiyo kwenye gazeti rasmi la serikali.

Hii kwa mujibu wa mbunge huyo itawarahisishia kupata kitambulisho.

“Jamii hii imepigana sana na imekuwa ikibaguliwa hasa vitambulisho vinapotolewa. Naomba Rais uangalie maslahi yao ili wapewe vitambulisho,” akasema Bw Orero anayehudumu muhula wa kwanza bungeni.

Akiongea katika Kaunti ya Kajiado, Katibu katika idara ya huduma kwa raia Julius Bitok aliahidi kutii amri ya Rais akiwataka wasiokuwa na stakabadhi hiyo waiendee.

“Kutokana na kauli ya Rais Ruto ningependa kuwaona wengi wakijitokeza kuchukua kitambulisho kwa sababu hakuna kulipa chochote. Hakuna mtu yeyote atakayekuomba pesa ukisaka kitambulisho,” akasema Balozi Bitok.

Hata hivyo, haijulikani iwapo amri ya rais pia itatekelezwa kwa wale ambao walikuwa na kitambulisho, wakakipoteza na wanasaka kingine.

Akiwa Kibra ambayo ni ngome ya Kinara wa Upinzani Raila Odinga, Rais alisema kuwa aliamua kushirikiana na waziri huyo mkuu wa zamani kwa ajili ya amani nchini.

Rais pia alitangaza kuwa serikali itatenga Sh40 milioni kwa upanuzi wa Taasisi ya Kiufundi na Mafunzo ya Kibra.