Ruto ahimiza wanasiasa wenzake wafikirie jinsi ya kuwatoa Wakenya katika umaskini
Na CHARLES WASONGA
NAIBU RAIS William Ruto amesema shida zilizosababishwa na ukabila ndizo zimechangia mamilioni ya Wakenya kuishi katika lindi la umaskini.
Kwenye ujumbe kupitia akaunti yake ya Twitter, Dkt Ruto alisema hali hiyo inaweza tu kurekebishwa ikiwa siasa za taifa hili zitabadilishwa na kukoma kuongozwa na ukabila bali haja ya kuimarisha hali ya maisha ya watu maskini.
Alisema tabaka la maskini, maarufu kama “husler” halijafungwa na minyonyoro ya ukabila bali haja ya kuwaondoa wenza zaidi ya 20 milioni wanaoishi katika hali ya ukata.
“Hatimaye tumekumbatia mjadala muhimu zaidi maishani mwetu; mjadala kuhusu hasla. Hadi sasa siasa zetu zimekuwa mateka wa ujinga wa ukabila na mtu wetu. Hii ni sababu ambayo imechangia karibu nusu ya Wakenya kuishi katika umaskini na wengine 16 milioni hawana ajira. Dhana ya hasla, ambaye hana kabila, imeleta mwamko mpya katika siasa zetu,” Dkt Ruto akasema kupitia Twitter.
Naibu Rais alionekanana kurejelea hatua ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kutaka kujinasibisha na tabaka la maskini, kwa kudai kuwa babake, Jaramogi Oginga Odinga pia alitoka familia maskini.
Akiongea mjini Kisumu Jumapili Bw Odinga pia alisema familia za Rais Uhuru Kenyatta, marais wa zamani Daniel Moi na Mwai Kibaki pia zilikuwa masikini hapo mbele.
“Mtu hawafai kuendeleza siasa za mahasla na kizazi cha matajiri viongozi. Hata marais wa zamani kama Moi na Mwai Kibaki waliinuka kutoka kwa umasikini mkubwa. Binafsi babu yangu alikuwa maskini kupindukia,” Bw Odinga akasema alipokuwa akihutubia wajumbe wa ODM kutoka kaunti ya Kisumu.
Dakika chache baadaye, akiongea baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa la AIC, Ziwani, Nairobi, Dkt Ruto alimwalika Bw Odinga katika tabaka la mahasla lakini akamshauri kuwa na moyo ya kuwasaidia wanyonge.
“Nimesikia mwingine akisema yeye pia ni hasla; namwambia karibu. Lakini namwomba kutathamini biashara ndogondogo zinazoendeshwa na sisi mahasla na awe tayari kutoa kile kidogo alichonacho kupiga jeki biashara hizo. Mungu hubariki mkono unaotoa kuliko ule unaopokea,” Dkt Ruto akasema.