HabariSiasa

Ruto akosekana katika uzinduzi wa Huduma Namba

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

BENSON MATHEKA, PETER MBURU Na BENSON AMADALA

NAIBU Rais William Ruto, Jumanne alikosekana kwenye shughuli za kuzindua usajili wa Wakenya kwa njia ya kielektroniki, maarufu kama Huduma Namba.

Dkt Ruto hakushiriki shughuli hiyo ambayo Rais Uhuru Kenyatta na viongozi wa upinzani Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula waliongoza maeneo mbalimbali ya nchi.

Rais Kenyatta aliongoza shughuli hiyo Machakos, Raila akazindua Mombasa, Kalonzo na Wetangula wakasimamia Murang’a naye Mudavadi akaongoza Kajiado.

Mawaziri kadhaa na viongozi wakuu wa serikali pia walikuwa mashinani kuzindua shughuli hiyo ambayo Rais Kenyatta aliitaja kama mwanzo wa kumaliza ukabila Kenya.

“Raila yuko Mombasa, Mudavadi yuko Kajiado, Kalonzo yuko Murang’a kujisajili kupata Huduma Namba. Hii ni siku muhimu ya kumaliza ukabila Kenya,” akasema Rais Kenyatta bila kumtaja Dkt Ruto.

Bw Odinga alipojisajili kwa Huduma Namba jijini Mombasa. Picha/ Hisani

Dkt Ruto alitarajiwa kuongoza shughuli hiyo eneo la Kambi la Mwanza, Kaunti ya Kakamega lakini hakufika na ikabidi Waziri wa Michezo, Amina Mohammed kuongoza hafla hiyo. Ililazimu ratiba ibadilishwe dakika za mwisho ilipofahamika kuwa hangefika.

Bi Mohamed aliandamana na Mawaziri Mwangi Kiunjuri (Kilimo), Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na Gavana Wycliffe Oparanya wa kaunti hiyo.

“Naibu Rais hangeweza kuwa nasi katika hafla hii kutokana na majukumu mengine ya kikazi aliyo nayo,” akasema Bi Mohamed.

Baadaye Dkt Ruto alituma ujumbe na picha kwenye Twitter, akiwa na ujumbe kutoka Cuba.

Rais Kenyatta alisema Huduma Namba itasaidia Wakenya kupata huduma za serikali kwa urahisi, kupunguza muda na gharama ya kupata huduma pamoja na kuondoa wafanyakazi hewa katika serikali.

Alisema serikali ilitumia usajili wa maafisa wa polisi kufanyia majaribio shughuli hiyo na ikagundua kwamba zaidi ya maafisa hewa 5,000 walikuwa wakipokea mshahara.

Rais Kenyatta alipozindua magari ya kufanikisha usajili wa Huduma Namba katika Kaunti ya Machakos Aprili 2, 2019. Picha/ Jeff Angote

“Kwa mwezi mmoja baada ya kuondoa maafisa hao hewa, tunaokoa zaidi ya Sh158 milioni,” alisema Rais Kenyatta.

Alisema wafanyakazi wote wa idara za serikali watasajiliwa ili kukabiliana na ufisadi ambao umekita kambi serikalini.

“Wale ambao wanapinga shughuli hii wanafanya hivyo kwa sababu wanajua watapatikana kupitia Huduma Namba,” akasema.

Baada ya kusajiliwa, Wakenya hawatakuwa wakibeba aina tofauti za vitambulisho wanapotafuta huduma tofauti. Rais Kenyatta alisema Huduma Namba pia itapunguza wizi wa vitambulisho.

“Huduma namba itapunguza ufisadi katika utoaji wa pesa za wazee na basari kwa watoto, pamoja na kurahisisha utoaji wa paspoti. Kupitia usajili huo, serikali pia itakuwa na rekodi sahihi kuweza kufuatilia maambukizi ya maradhi na majeraha yanayoua watu nchini,” alisema Rais Kenyatta.

Rais alisema sajili ambayo serikali itaandaa itakuwa ikitumiwa kufuatilia idadi ya watu kwa sababu itaweka rekodi za watoto wanaozaliwa na idadi ya watu wanapokufa.

Rais Kenyatta awaeleza wakazi wa Machakos manufaa ya Huduma Namba katika kituo cha usajili. Picha/ Jeff Angote

Sajili hiyo, alieleza Rais, itasaidia serikali kutekeleza Ajenda Nne Kuu.

Kwenye hotuba yake, Rais alisema kwa kusajili Wakenya kwa njia ya kielekroniki, Kenya itajiunga na mataifa mengine ulimwenguni yanayoweka rekodi za habari muhimu za raia wake.

Kila Mkenya atahitajika kutumia kitambulisho chake cha kitaifa ama cheti cha kuzaliwa kujisajili kupata Huduma Namba.

Alifichua kuwa Huduma Namba itasaidia serikali katika vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelea. “Kupigana na ufisadi sio suala la mtu kuombwa kufanya uamuzi. Ni suala la lazima na kila mmoja anafaa kujiunga na vita hivi,” alisema.

Kuhusu hofu ya usalama wa habari za watu binafsi zitakazokusanywa kwenye shughuli hiyo, Rais Kenyatta alisema serikali inaandaa sheria ambayo itathibiti upatikanaji wa habari kuhusu mtu binafsi.

“Tuko mbioni kuandaa sheria ambayo itathibiti usambazaji wa habari na kuhakikisha kwamba habari hizo zimelindwa,” alisema Rais.

Mnamo Jumatatu mahakama ilizuia serikali kujumuisha rekodi za chembechembe za damu maarufu kama DNA kwenye usajili huo. Aidha, mahakama iliagiza serikali kutotoa habari hizo itakazokusanya shirika au mataifa mengine.