Ruto alimbikiza ahadi Jamhuri Dei
RAIS William Ruto jana aliendelea kutoa ahadi kuhusu hatua muhimu za kugeuza Kenya kuwa taifa lenye uchumi wa kisasa na uhuru wa kiuchumi kwa wananchi wote.
Rais Ruto alisema kuwa marekebisho ya sera za kiuchumi yamesaidia kuimarisha uchumi, kurejesha imani ya wawekezaji, na kuongeza thamani ya sifa ya mkopo wa taifa.
Hii ni sehemu ya mpango wa Sh 5 trilioni unaolenga kufanikisha nchi kuwa ya uchumi wa kiwango cha kwanza.
Rais Ruto alitaja hatua tatu kuu zinazounda msingi wa mpango wake wa taifa.
Serikali imepanga mradi wa miaka 10 wa barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na mabomba ya mafuta, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa barabara kuu za miji mikuu na kuunganisha mashamba, viwanda, na masoko.
Hivi karibuni, serikali ilizindua ujenzi wa barabara ya Nairobi–Nakuru–Mau Summit na Nairobi–Maai Mahiu–Naivasha, mradi wenye thamani ya KSh 180 bilioni.
“Wiki iliyopita, wananchi wenzangu, tulichukua hatua kutoka kwa ahadi hadi utekelezaji kwa kuanzisha ujenzi wa barabara ya Nairobi–Nakuru–Mau Summit na Nairobi–Maai Mahiu–Naivasha, uwekezaji wa zaidi ya Sh180 bilioni katika barabara ya kisasa,” alisema.
Aidha, serikali imepanga kujenga barabara kuu za kilomita 2,500 ili kuunganisha kaunti zote 47, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na wananchi, na kuimarisha uchumi wa viwanda na kilimo.
Upanuzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Malaba, pamoja na upanuzi wa bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, pia umekusudiwa kufungua njia mpya za usafirishaji ndani ya nchi na kieneo.
‘Mnamo Februari 2026, tutaanza kupanua Reli ya Kisasa kutoka Naivasha hadi Malaba, na mwishoni mwa mwaka, kupanua bomba la mafuta kutoka Eldoret kwenda Uganda, kufungua mlango mpya wa usafirishaji na majirani zetu na bara lote,’ alisema.
Katika hotuba yake Rais Ruto alianika mikakati na ahadi za serikali yake zinazolenga kuimarisha uchumi wa Kenya na kufanikisha uhuru wa kiuchumi.
Rais aliahidi barabara ya Expressway kutoka Thika hadi Museum Hill kuanzia mwaka ujao, akisema hatua hiyo itapunguza msongamano wa magari mjini Nairobi.
‘Kuna mambo mengi tuliyokubaliana na Serikali ya Kaunti ya Nairobi kuendeleza mjini. Tutajenga barabara zote ambazo zilikuwa zimekwama hapa Nairobi, na tayari tumeafikiana kurudisha wakandarasi wote,’ alisema Ruto.
Rais pia alibainisha kuwa kilomita 60 za barabara tayari zinaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali jijini.
“Kuanzia Desemba hii, wakati mtakuwa mnasafiri kwa Krismasi, tutajenga upya barabara kutoka JKIA hadi ABC na kupamba jiji ili Nairobi ionekane kama mji wa kisasa,’ alisema.
Ruto pia aliahidi upanuzi wa eneo la Nairobi Metropolitan, akilenga sehemu ambazo wakazi wanakabiliwa na msongamano mkubwa kila siku.
‘Tunajua Wakenya wengi wanaishi ndani ya eneo la Nairobi na kufanya kazi mjini—watu wanaoishi Kiserian, Rongai, Ngong—wanaopitia msongamano mkubwa asubuhi na jioni.
Kuanzia mwaka ujao, barabara kutoka Bomas of Kenya hadi Rongai na Kiserian, na kutoka Karen kupitia Ngong hadi Kiserian, itapanuliwa,’ alisema.
Akitaja barabara ya Thika, Rais alisema: ‘Ninaelewa kuwa watu wengi wanaoishi Thika na kutumia Thika Road wanakabiliwa na msongamano mkubwa.
Kuanzia mwaka ujao, kama ilivyo Expressway kutoka JKIA, pia tutajenga Expressway kutoka Thika hadi Museum Hill ili kupunguza msongamano.’
Rais Ruto pia alitaja mipango ya kuboresha bandari za Mombasa na Lamu na viwanja vya ndege vya kitaifa, ikiwemo JKIA, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa, watu na huduma, na kufanya Kenya iwe kitovu cha biashara kanda nzima.
Alisisitiza kwamba miradi hii yote itapunguza gharama za usafirishaji, na kuunda fursa mpya za biashara na uwekezaji.
Kuhusu kilimo na utoshelevu wa chakula, Rais Ruto aliahidi mabwawa makubwa 50, madogo 200, na madogo zaidi 1,000 katika kaunti zote, hasa katika maeneo kame na nusu kame.
Miradi hii inalenga kuongeza ardhi inayopandwa chakula, kuongeza uzalishaji wa chakula, na kuwezesha Kenya kuzalisha bidhaa za kilimo na viwandani.
“Hii si tu utoshelevu wa chakula na maji, bali ni uwekezaji unaoathiri taifa mzima,” alisema.
Katika sekta ya kawi, Rais Ruto alitaja mipango ya kuongeza uzalishaji wa kawi hadi Megawati 10,000 katika miaka saba ijayo. Kenya ina rasilmali kubwa za kawi endelevu.