Habari

Ruto aomba korti itupe kesi ya kumtimua mamlakani

Na JOSEPH WANGUI March 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ameitaka mahakama moja ya Nairobi kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu wakitaka aondolewe mamlakani kupitia kura ya maamuzi.

Kulingana na wanaharakati hao, Rais Ruto amedhihirisha utepetevu kazini, ametumia vibaya mamlaka huku akikiuka Katiba na hivyo hafai kuendelea kushikilia wadhifa huo kwa niaba ya Wakenya.

Kundi la mawakili wa Rais, wakiongozwa na wakili mkuu Fred Ngatia, wanasema kuwa kesi hiyo inasheheni dosari nyingi na inastahili kutupiliwa mbali.

Wakili huyo aliangazia masuala kadha ya kisheria yakiwemo kumshtaki rais kama mtu binafsi na uhalali wa mbinu inayopendekezwa ya kumwondoa rais mamlakani, kupitia kura ya maamuzi.

Alipofika mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye Jumanne, Bw Ngatia alisema kuwa kesi hiyo inatwaa mamlaka ya kikatiba iliyotwikwa Bunge la Kitaifa la kumwondoa mamlakani rais.

“Ombi hili halina msingi wowote na linaenda kinyume na Kipengele cha 143 (2) cha Katiba,” akasema Bw Ngatia.

Kipengele hicho kinasema kuwa rais aliye mamlaka hawezi kushtakiwa kama mahakama yoyote kutokana na kitu chochote alichofanya akitekeleza majukumu ya afisi hiyo.

Kesi hiyo iliwasilishwa na wanaharakati 13 wa kutetea haki za kibinafamu na shirika la kijamii la Kenya Bora Tuitakayo Citizens Association mnamo Agosti mwaka jana.

Wanaharakati hao wanataka mahakama kuu itoe uamuzi kuwa muhula wa kuhudumu wa Rais Ruto unaweza kukatizwa kabla ya miaka mitano kutamatika.

Walalamishi wanataka Mahakama Kuu kuagiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iandae kuwa ya maamuzi kuamua ikiwa muhula wa rais unaweza kukatizwa kwa misingi ya ukiukaji wa katiba, matumizi mabaya ya mamlaka yake na utepetevu.

Kando na hayo, wanaharakati hao wanadai kuwa Rais alitumia vibaya mamlaka kwa kuzingatia ukabila kama kigezo anapoteua maafisa wakuu serikalini.

Lakini kulingana na wakili Ngatia, walalamishi hao wanatoa mapendekezo ambayo “hayajawahi kutolewa”na hivyo ombi lao linapasa kutupiliwa mbali.

“Kuondolewa afisini kwa rais chini ya Katiba ya Kenya kunaweza kufanikishwa na Bunge la Kitaifa pekee kwa misingi sababu zilizoorodheshwa katika vipengele vya 144 na 145 vya Katiba,” akasema Bw Ngatia.