Ruto apewa fursa ya kuajiri makamishna wa IEBC kihalali
MAHAKAMA imekosoa hatua ya Rais William Ruto kuajiri makamishna wapya wa IEBC bila idhini ikisema agizo la mahakama lililokuwepo lilistahili kuheshimiwa.
Hata hivyo, korti hiyo wakati huo huo imetupa kesi iliyotaka uteuzi mzima ufutwe, jambo linalotoa nafasi kwa Rais kuwaajiri kihalali.
Majaji Roseline Aburili, John Chigiti na Bahati Mwamuye walimkosoa vikali Bw Ruto kwa kuajiri Erastus Ethekon Edung na wenzake wakati ambapo kulikuwa na agizo la mahakama la kusitisha zoezi hilo hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani isikizwe na kuamuliwa.
Majaji hao hata hivyo walisema hawakupata ithibati yoyote kwamba uteuzi mzima umekiuka katiba. Kwamba madai ya walalamishi kwamba uteuzi haukufikisha vigezo vya usawa wa kimaeneo hayakuwa na mashiko na kwamba malilio walalamishi waliyotaka hayakuwiana na madai waliyowasilisha.
Ikimkosoa Dkt Ruto kwa kupuuza mahakama, korti hiyo ilisema maagizo yake hayatolewi ili kukaidiwa na yeyote ikisema Rais alipaswa kusubiri tu hadi kesi iamuliwe ndipo afanye uajiri rasmi. Ni kwa sababu hiyo ilifutilia mbali tangazo la Gazeti Rasmi lililotolewa na Serikali la kuajiri Bw Edung na wenzake sita.
Ingawa hivyo, hatua ya mahakama kuamua kesi iliyokuwa imepinga uteuzi wa makamishna hao inamaanisha kwamba Rais ana fursa sasa ya kuajiri saba hao kihalali wakati wowote sasa.