Habari

Ruto apiga Raila dafrau

April 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA na DPPS

NAIBU RAIS William Ruto, Jumanne alimpiga dafrau kinara wa ODM, Raila Odinga kwa kumshawishi mgombeaji wa chama hicho kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Wajir Magharibi ajiondoe.

Hii imetokea siku chache tu baada ya habari kudokeza kuwa Dkt Ruto alihusika katika kampeni za Justus Mawathe na David Ochieng walioshinda wagombeaji wa ODM Embakasi Kusini na Ugenya mtawalia, wiki iliyopita.

Mgombeaji huyo wa Wajir Magharibi, Yussuf Elmi, alitangaza kujiondoa kwake akiwa nyumbani kwa Dkt Ruto mtaani Karen jijini Nairobi, saa chache baada ya ODM kutoa taarifa ikisema ndiyo iliyochukua uamuzi wa kujiondoa kwenye uchaguzi huo.

Duru zilidokeza kuwa ODM kilichukua hatua za haraka kutangaza kujiondoa kilipopata habari kuwa Prof Elmi alikuwa anakutana na Dkt Ruto, na angejiondoa kwenye uchaguzi huo.

Duru zilidokeza kuwa ODM kilichukua hatua za haraka kutangaza kujiondoa kilipopata habari kuwa Prof Elmi alikuwa anakutana na Dkt Ruto, na angejiondoa kwenye uchaguzi huo.

“Leo nimejiondoa katika uchaguzi mdogo wa Wajir Magharibi. ODM haihusiki kwa vyovyote na uamuzi wangu,” akasema Prof Elmi.

Dkt Ruto naye alikanusha kuwa kujiondoa kwa Prof Elmi kulikuwa na nia ya kuunga mkono mgombeaji wa Jubilee, Ahmed Kolosh.

Awali kabla ya Prof Elmi na Dkt Ruto kuzungumza, ODM kilikuwa kimedai kilichukua hatua hiyo kwa moyo wa handisheki, baada ua kushauriana na wakuu wa Jubilee.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Junet Mohammed, alisema chama hicho kilifikia uamuzi huo baada ya kushauriana na uongozi wa Jubilee.

“Tumekubaliana kurudisha mkono kufuatia hatua ya awali ya Jubilee ya kujiondoa kutoka chaguzi ndogo za Migori, Ugenya na Embakasi Kusini,” akasema Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ODM, Junet Mohammed.

Kauli ya Prof Elmi kuwa uamuzi wake haukuhusisha ODM, inaashiria chama hicho kilitoa taarifa ya uongo, wakati ambapo kinakumbwa na aibu ya kushindwa kwenye chaguzi ndogo Embakasi Kusini na Ugenya wiki ilyopita.

“ODM kingetaka kujiondoa katika kinyang’anyiro cha Wajir Magharibi baada ya kuingiza baridi kufuatia kushindwa katika chaguzi za wiki jana katika Embakasi Kusini na Ugenya. Hii ndio maana Raila amechukua hatua hiyo,” mchanganuzi wa siasa, Bw Martin Andati aliiambia Taifa Leo kabla ya Prof Elmi kutoa taarifa yake.

Uchaguzi huo wa Wajir Magharibi uliitishwa baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali ushindi wa Bw Kolosh, ambaye alikuwa ameshinda kiti hicho kwa tiketi ya ODM katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Lakini sababu ilizotoa ODM za kujiondoa zilionekana zisizo na msingi ikizingatiwa kuwa tayari walikuwa na mgombeaji, Prof Elmi, kinyume na Jubilee ambayo haikuweka mgombeaji yeyote katika chaguzi za Migori mwaka jana pamoja na Embakasi Kusini na Ugenya mwaka huu.

Pia wakati ambao hatua hiyo imechukuliwa unaonyesha kuwa imetokana na aibu ambayo chama hicho kilipata kwenye chaguzi za Embakasi Kusini na Ugenya.

Kushindwa kwa ODM hasa Ugenya kumeonekana kama ishara ya kufifia kwa umaarufu wake na wa Bw Odinga, na hivyo chama hicho kilichukua hatua ya kujiondoa Wajir Magharibi kuzuia aibu zaidi.

Bw Odinga alisema mnamo Jumatatu kuwa kushindwa kwa ODM kwenye chaguzi hizo sio jambo kubwa.

Bw Kolosh alipokelewa rasmi na Dkt Ruto katika Jubilee mnamo Februari 22.