HabariSiasa

Ruto atanipigia magoti – Kutuny

September 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

GERALD BWISA na DENNIS LUBANGA

NAIBU wa Rais William Ruto ameanza harakati za kutaka kumng’oa kitini mbunge wa Cherang’any, Joshua Kutuny, 2022.

Bw Kutuny, kwa upande mwingine, ameapa kumpa kipigo cha kisiasa Naibu wa Rais Dkt Ruto ambaye ametangaza azma yake ya kuwania urais 2022.

Bw Kutuny amemshutumu Naibu wa Rais kwa kushindwa kushughulikia masilahi ya jamii ya Wakalenjin licha ya kushikilia wadhifa wa juu serikalini.

“Wakulima wa mahindi wanahangaika na kulazimishwa kukuza mazao mbadala kujikimu kimaisha. Hii ni ishara kwamba Naibu wa Rais ametelekeza jamii ya Wakalenjin,” akasema Bw Kutuny katika mahojiano na Taifa Leo, Jumamosi.

“Hivi majuzi (Dkt Ruto) alikuwa katika eneobunge langu na anafaa kujua kwamba nitafunza somo la kisiasa ambalo hawatasahau maishani mwake. Wakati wa wanasiasa kutumia uongo kuwadanganya Wakenya umeisha,” akasema Bw Kutuny.

Kulingana na Bw Kutuny, kuna wanasiasa wengi humu nchini wanaoweza kumbwaga dkt ruto katika uchaguzi mkuu wa 2022.

“Amekuwa (Ruto) akizunguka katika eneobunge langu akisema kuwa atahakikisha kuwa ninafeli 2022. Anadhani kwamba hakuna viongozi wengine humu nchini wanaoweza kumbwaga,” akasema Bw Kutuny ambaye ni mshauri wa zamani wa masuala ya kisiasa wa Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Kutuny alijutia kwa nini alimpigia kampeni Naibu wa Rais Dkt Ruto katika chaguzi zilizopita.

“Ninajutia kushirikiana na Dkt Ruto katika chaguzi zilizopita. Ajiandae kwani kuporomoka kwake kisiasa kunakaribia. Hivi karibuni atakuja kuniomba masamaha,” akasema mbunge huyo anayechukuliwa kuwa mwasi.

Dkt Ruto amekuwa akishutumu Bw Kutuny kwa ‘kutumiwa’ na watu kutoa nje kutatiza azma yake ya kutaka kuingia ikulu 2022.

“Ikiwa anadhani (Ruto) ataniangusha kisiasa basi nitamwaibisha kisiasa. Ninamfahamu vyema na hivi punde nitamwonyesha kivumbi,” akasema mbunge huyo wa Jubilee.

Ijumaa wakati wa mazishi ya aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni ya maziwa ya KCC Kibiwot Koros kijijini Birbiriet, eneobunge la Cherangany, Ijumaa iliyopita, Naibu wa Rais alisema Bw Kutuny ametelekeza majukumu yake na sasa anahudumiwa watu fulani jijini Nairobi.

Dkt Ruto alisema kwamba atahakikisha kuwa anawahudumia wakazi wa Cherangany baada ya kutelekezwa na mbunge wao (Bw Kutuny).

“Inasikitisha kwamba mtu ambaye alichaguliwa na wapigakura awatumikie, ameenda Nairobi kunywa na kula na watu ambao hawana haja na maendeleo ya eneo hili.

“ Sasa amepewa mkuki wa kuwarushia watu wake. Kwa sababu mlinichagua pamoja na Rais Kenyatta sitawasahau, nitawatumikia,” akasema Dkt ruto.