Ruto atimiza ahadi, awapa wavuvi wa Homa Bay Sh5 milioni alizowaahidi
WAVUVI katika Kaunti ya Homa Bay wana sababu ya kutabasamu baada ya Rais William Ruto kutimiza ahadi ya kuwapa Sh5 milioni kupi jeki akiba yao.
Wavuvi hao walipokea fedha hizo kutoka kwa Rais Jumanne.
Fedha hizo ziliwasilishwa kwa kikundi hicho na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga katika hafla moja.
Alipokuwa ziarani kwenye Kaunti hiyo mnamo Mei 30 kabla ya Madaraka Dei, Rais alikutana na usimamizi wa chama cha wavuvi hao cha akiba na mikopo na akawaahidi kuwapiga jeki.
Hii ilikuwa baada ya wavuvi hao kuambia Dkt Ruto kwamba walikuwa wameanzisha chama cha akiba na mikopo na kwamba walihitaji usaidizi ili kutimiza malengo yao.
Wakati wa mkutano huo, Rais alisema alikuwa makini kuboresha uchumi wa baharini na maji makuu.
Bi Wanga alithibitisha kwamba Rais alimpa pesa hizo ambapo alienda kuzihifadhi benki.
“Kuna watu wanasema Rais hatimizi ahadi anazotoa. Lakini tuko hapa kuthibitisha kwamba yeye hutimiza na leo tunapeana pesa ambazo aliahidi atawapa wanachama wa BMU Homa Bay,” akasema gavana huyo.