Ruto aunga mkono amri ya Trump ya kutotambua watu wenye jinsia mbili almaarufu huntha
RAIS William Ruto ameunga mkono amri ya Rais wa Amerika Donald Trump ambayo inatambua tu jinsia mbili; ile ya kike na ya kiume.
Kiongozi wa nchi Jumapili alisema anaunga mkono hatua ya Rais Trump kuwapiga marufuku huntha (watu wenye jinsia mbili) kuhudumu kwenye jeshi la Amerika. Amri ya Rais Trump iliyotiwa saini mnamo Januari 2021 ilisema kuwa serikali itatambua tu jinsi mbili.
“Kinyume na kile ambacho kimekuwa kikifanyika, mara hii tumeshuhudia mabadiliko mazuri Amerika. Wamekumbatia sera ambazo tumekuwa tukishabikia kwa sababu wanaume watasalia wanaume nao wanawake wawe tu wanawake,” akasema Rais Ruto.
“Tunamshukuru Mungu kwa mwaka huu kwa sababu habari kutoka utawala mpya wa Amerika zinaonyesha kile ambacho kimeandikwa kwenye bibilia sasa kinaaminika. Utamaduni wetu na imani yetu imeangaziwa na kuheshimwa,” akaongeza.
Alikuwa akiongea kwenye ibada ya Kanisa la Global Cathedral iliyofanyika ukumbi wa KICC Jumapili. Alisema Kenya inaunga mkono amri ya Rais Trump na kusema kuwa kuna uhusiano spesheli kati ya Amerika na Kenya.
Rais Ruto pia alikaribisha hatua ya Rais Trump kuunga mkono polisi Wakenya ambao wapo Haiti kusaidia kurejesha nchi hiyo kwenye mkondo wa utawala nzuri.
“Mwaka jana niliombwa na Rais Biden nisaidie kurejesha amani Haiti kwa kutuma vikosi vya polisi. Nimefurahi kuwa utawala wa Rais Trump unaunga mkono kazi ambayo tunafanya Haiti ili nchi hiyo iwe na amani,” akasema Rais.
Kenya mwaka jana iliahidi kutuma maafisa 1,000 wa polisi ili kusaidia utawala wa Haiti kupambana na magenge hatari. Kenya tayari ina polisi 400 jijini Port-au-Prince ambao wanasaidia katika kupambana na magenge.
Mnamo Januari 19 polisi wengine 217 walitua Haiti na wakapokolewa na Waziri Mkuu Alix Didier Fils-Aime, ambaye ni mshauri wa Rais Fritz Alphonse Jean na Kamanda Mkuu wa Misheni ya Kenya Haiti Godfrey Otunge.
Nchi 10 zimeahidi kuwatuma vikosi 3,100 vya walinda usalama Haiti japo ni nchi chache sana ambazo zimefanya hivyo hadi leo.
Maafisa hao waliandamana na aliyekuwa Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinett, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli na Ranson Lolmodooni ambaye ni kamanda wa kikosi cha GSU.
Polisi kutoka Kenya baadaye walipigwa jeki kwa kuwasili kwa raia 24 wa Jamaica na polisi wawili wa ngazi ya juu kutoka Belize. El Salvador mnamo Agosti mwaka jana iliahidi kuwatuma wanajeshi 78 na helikopta.
Rais Ruto aliwarai Wakenya waiombe serikali hii akisema kuwa mwaka huu utakuwa wa ufanisi.
“Kuna kila dalili kuwa Mungu anaibariki nchi yetu. Jana tu, tulipokea habari kuhusiana na kile Mungu anafanya kuponya taifa letu,” Rais akawaambia waumini.
“Kufanya kazi pamoja kumepunguza riba, bei ya bidhaa zimechuka, sarafu yetu imekuwa na thamani kwenye soko la hisa. Nakubaliana na askofu Moses Turere kuwa 2025 utakuwa mwaka wenye heri,” akasema.