Ruto awakemea wanaobashiri atapoteza kiti 2027
RAIS William Ruto amewakashifu wapinzani wake wanaobashiri kuwa atahudumu kwa muhula mmoja pekee akisema rekodi yake ya maendeleo ndiyo itamwezesha kushinda tena 2027.
Akiongea Jumapili alipohudhuria ibada katika Kanisa la United Pentecostal Church of Kenya eneo bunge la Dagoretti Kaskazini, alielezea matumaini kuwa atawashangaza mahasidi wake alivyofanya 2022 kwa kuwania kwa mara ya kwanza na kushinda.
“Nasikia wengine wakiongea kuhusu muhula mmoja, muhula wa pili au muhula watu. Nawaambia kwamba hapo awali, walisema kuwa sitashinda urais. Lakini nimefurahi kuwa Mungu alinipa nafasi ya kuwa Rais wa Kenya,” akasema.
“Mungu aliniwezesha kushinda urais licha ya kwamba natoka familia kidogo ambayo haijulikani hapa Kenya. Mungu amenipa nafasi ya kuleta mabadiliko nchini Kenya, nitafanya hivyo na Wakenya watanipa nafasi nyingine wakati ukitimu,” Dkt Ruto akaongeza.
Huku akiorodhesha mafanikio ambayo serikali yake imefikia katika nyanja ya uchumi, afya, elimu na uzalishaji nafasi za ajira, kiongozi wa taifa alisisitiza kuwa Wakenya watamchagua tena kwa misingi ya rekodi hiyo.
“Inasikitisha kuwa watu wengine wameshindwa kuona kuwa bei za bidhaa za kimsingi kama unga na mafuta zimeshuka ikilinganishwa na 2022, thamani ya shilingi ya Kenya imeimarika dhidi ya dola, nyumba za gharama nafuu zinajengwa na vijana wamepata ajira na bima mpya ya afya inafanya kazi,” Dkt Ruto akaeleza.
Rais alionekana kuwajibu wandani wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambao juzi walibashiri kuwa ataanguka katika uchaguzi mkuu ujao.
“Kutokana na maovu yanayoshuhudiwa nchini wakati huu kama vile utekaji nyara wa watu kiholela, ufisadi, unyakuzi wa ardhi na kupanda kwa gharama ya maisha, hamna Mkenya mwenye akili timamu atamchagua tena William Ruto 2027. Ataweka historia kwa kuwa rais aliyehudumu kwa muhula mmoja pekee,” Seneta wa Kiambu Karungo Thang’wah akawaambia wanahabari Westlands, Nairobi.