Habari

Ruto awashauri wakulima kukumbatia mbinu za kisasa

February 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto ametoa wito kwa wakulima nchini kukumbatia mbinu za kisasa ili kuchuma faida kwa gharama ya chini.

Alisema nyakati ambapo kilimo kilikuwa kikiendeshwa kama ada, kwa kuzingatia mbinu za kizamani, zimepitwa na wakati kwani sasa shughuli hiyo inapaswa kuendeshwa kama biashara.

“Serikali imepata masoko ya mazao ya kilimo katika mataifa ya Ulaya na Bara Asia. Hivi karibuni tutakamilisha mkataba ambao utawezesha wakulima wa kahawa kupata masoko ya kahawa na chai katika maeneo hayo,” akasema Ruto akiwa mjini Karatina alipohudhuria hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kufariki kwa Gavana wa kwanza wa Nyeri, Nderitu Gachagua.

Dkt Ruto alikuwa ameandamana na Spika wa Seneti Ken Lusaka, magavana Ferdinand Waititu (Kiambu) na Mutahi Kahiga (Nyeri).

Pia walikuwapo wabunge; Munene Wambugu (Kirinyaga ya Kati), David Njuguna (Olkalou), Kimani Ichungwa (Kikuyu), Nelson Koech (Belgut), Caleb Kositany (Soy), Rigathe Gachagua (Mathira), Rahab Mukami (Mbunge Mwakilishi, Nyeri), Kabinga Wachira (Mwea), Jayne Kihara (Naivasha), Oscar Sudi (Kapseret), Moses Kuria (Gatundu Kusini) na Rehema Jaldesa (Mbunge Mwakilishi, Isiolo).

Kuongeza thamani

Naibu Rais aliwataka wakulima wa kahawa kuongeza thamani kwa zao hilo ili kuweza kupata mapato mazuri.

“Hii ndio njia ya kuongeza mapato kwa wakulima wetu pamoja na kuzalisha nafasi zaidi za ajira,” Dkt Ruto akaongeza.

Alisema serikali tayari inawasaidia wakulima kuongeza thamani kwa maziwa yao kupitia mpango wake wa usambazaji mitambo ya kuhifadhi maziwa yasiharibike haraka (cooling plants).

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo walitoa wito kwa serikali kuendeleza vita dhidi ya maradhi ya kansa ambayo walisema imegeuka janga la kitaifa.

“Sisi kama viongozi tunapaswa kuwahimiza wananchi kutumia vifaa vilivyotumwa katika kaunti kwa ajili ya kuchunguza kansa,” akasema Mbunge wa Mathira Ragathi Gachagua.

Bw Gachagua ni kakake mdogo marehemu Gavana wa zamani wa Nyeri Ndiritu Gachagua ambaye alifariki baada ya kuugua kansa kwa kipindi kirefu.

Kwa upande  wao, Bw Lusaka na Gavana Kahiga waliwataka wanasiasa kuendelea kuiunga mkono serikali katika mchakato wake wa kutekeleza Ajenda Nne Kuu za serikali.