Ruto awasili Rongai kwa mazishi ya Kenei
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto amewasili Chamasis, Solai, Rongai, Kaunti ya Nakuru kwa mazishi ya marehemu Sajini Kipyegon Kenei.
Hadi kifo chake majuma mawili yaliyopita, mwendazake alikuwa mkuu wa walinzi katika Afisi ya Naibu Rais katika Jumba la Harambee, Nairobi.
Alipatikana ameuawa nyumbani kwake Nairobi.
Waziri wa Leba Simon Chelugui ambaye ni binamuye marehemu, amempokea Naibu Rais katika kijiji cha Chamasis, wadi ya Solai.
Mnamo Februari 20, 2020, maiti ya Kenei ilipatikana nyumbani kwake katika mtaa wa Imara Daima, ikiwa na majeraha ya risasi kichwani.
Mwanzoni maafisa wa polisi walitangaza kuwa alijitoa uhai, lakini mnamo Alhamisi Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti alisema kuwa uchunguzi ulioendeshwa na maafisa wake umebainisha kuwa Sajini Kenei aliuawa kinyama.
Inadaiwa kuwa kifo chake huenda kilitokana na sakata ya utoaji zabuni feki ya ununuzi wa silaha, ya kiasi cha Sh39.4 bilioni inayomhusisha aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa.
Dkt Ruto amemtaka Bw Kinoti na maafisa wake wakamilishe uchunguzi haraka na wawapate wale waliomuua Kenei huku akimtaka “kukomesha sarakasi zisizo na msingi wowote.”
Hii ni baada ya Bw Kinoti kutoa picha za kamera za usalama, CCTV, zikionyesha jinsi Bw Echesa alivyoingia katika afisa za Dkt Ruto za Harambee Annex na wageni wawili kujadili zabuni hiyo.
“Sharti ukweli upatikane kuhusu sababu, namna na ni nani aliyemuua Sajini Kenei. Familia, Afisi ya Naibu Rais na Wakenya wanataka uikweli na haki na wahalifu waadhibiwe kwa mujibu wa sheria. Hizi drama, upotoshi, uongo na kampeni za kuharibu sifa zinazoendeshwa katika vyombo vya habari ni sawa na kufunika ukweli,” Dkt Ruto akasema kupitia chapisho lake katika ukurasa wa mtandao wa Twitter.