Ruto bado anawapenda, katibu wa wizara aambia ‘watu wa Mulima’
KATIBU katika Wizara ya Afya Mary Muthoni amesema kuwa Rais William Ruto bado analienzi eneo la Mlima Kenya na atahakikisha kuwa miradi yote aliyoahidi wakazi wakati wa kampeni inakamilishwa.
Kwa mujibu wa Bi Muthoni, Rais Ruto anatimiza ahadi aliyotoa wakati wa uchaguzi wa 2022 wala hatafanya maendeleo kwa sharti kuwa lazima aungwe mkono 2027.
“Watu wetu kumbukeni tulimpigia rais kura na bado anaendelea kutimiza ahadi alizotoa. Ukituangalia, amini kuwa tuko serikalini na tunawatakia watu wetu mazuri katika serikali,” akasema Bi Muthoni.
Alikuwa akiongea katika Kaunti ya Kirinyaga wikendi wakati wa kikao na umma kuhusu miradi ya serikali.
Kikao hicho kilishirikisha maafisa wa serikali ambapo waliangazia miradi ambayo ilikamilishwa eneo la Mlima Kenya na ile ambayo inastahili kukamilishwa.
Kila afisa aliyezungumza kwenye mkutano huo, alisema wajibu ambao ameutekeleza ni kuhakikisha kuwa kura za 2022 za Mlima Kenya zinapata thamani kupitia miradi ya maendeleo.
“Tuko pazuri kuhakikisha kuwa bei ya majanichai na kahawa inapanda kwa sababu ndiyo misingi ya uchumi wa watu wa eneo hili. Serikali itafanya juu chini kuimarisha bei ya mazao ya wakulima wetu,” akasema Lucy Njeri ambaye ni afisa wa Serikali kutoka Mamlaka ya Uzalishaji wa Vyakula (AFA).
“Wiki ijayo tutaanza kuwasajili wakulima kama njia ya kuwafundisha kuhusu mbinu mpya ya kuwahi soko la Ulaya,” akaongeza.
Bi Muthoni aliwataka wakazi kutathmini miradi ambayo imetekelezwa na serikali na kuwaepusha wanasiasa ambao wanaeneza madai ya uongo dhidi ya serikali.
Kuhusu afya, Bi Muthoni alipigia debe Bima ya Afya ya Jamii akisema kuwa inafanya kazi huku akiwakosoa baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakisema SHA ilifeli.
Msemaji wa serikali Isaac Mwaura aliwahakikishia wakazi wa Kirinyaga kuwa serikali inamakinika kutimiza ahadi ilizotoa.
Hata hivyo, alionya kuwa Mlima Kenya huenda ukapoteza mengi iwapo viongozi watakuwa wakishiriki siasa kila mara.
“Mwaka wa 2027 ni mbali na ni vyema iwapo tutaendelea kuunga mkono serikali ya sasa ili tunufaike baadaye. Najua rais anapenda sana eneo hili,” akasema Bw Mwaura.