Habari

Ruto: Hatuna mpango wa kuvuruga Elimu

Na DANIEL OGETTA July 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto amehakikishia Wakenya kwamba utawala wake unachukulia kwa uzito mkubwa ufadhili wa elimu bila malipo licha ya hofu ya mgao kwa shule kupunguzwa.

Akizungumza Jumapili, Julai 27, 2025 katika kanisa la Kianglikana la St Martins, Kariobangi, Nairobi, Rais alisisitiza kwamba elimu ingali nguzo kuu ya kitaifa.

“Nataka kuhakikishia kila mtu kwamba elimu haitaborongwa. Hatuwezi kuhatarisha upatikanaji wa elimu ya ubora wa juu na hatuwezi kudhalilisha umuhimu wa elimu,” akasema.

Matamshi yake yanajiri wakati kuna mjadala mkubwa uliosababishwa na kukiri mbele ya Bunge kwa Waziri wa Fedha John Mbadi kwamba serikali imepunguza mgao wa fedha kwa kila mwanafunzi kutoka Sh22,244 hadi Sh16,428 (upungufu wa Sh5,340) huku pia akisema Serikali inalemewa kufadhili Elimu Bila Malipo kikamilifu.