Habari

Ruto na Raila wasaidie kupunguza mihemko nchini – Kabogo

October 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

ALIYEKUWA Gavana wa Kaunti ya Kiambu William Kabogo amesema Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga ndio wanaoweza kupunguza au kutuliza joto la kisiasa linaloendelea kushuhudiwa nchini.

Bw Kabogo amesema hayo Jumatano, akilaani ghasia za wikendi Murang’a zilizosababisha vifo vya watu wawili.

Amesema anaamini viongozi hao wakikubali salamu za maridhiano (handisheki) kati yao, mihemko inayoshuhudiwa nchini itapungua.

Gavana huyo wa zamani pia amesema hafla za kisiasa zinazoandaliwa na viongozi hao maeneo tofauti nchini, zinaashiria mwanzo wa kampeni za mapema kuwania urais.

Hata ingawa kiongozi wa ODM Raila Odinga hajaweka wazi azma yake kuwania urais 2022, wandani wake wamekuwa wakidai atakuwa debeni kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Naibu Rais, Dkt William Ruto ameweka wazi nia yake kuingia Ikulu 2022.

“Watu ambao wanaweza kutuliza joto la kisiasa nchini ni Raila Odinga na William Ruto. Wafanye hivyo kwa kuzungumza na kuondoa tofauti kati yao, kisha Rais Kenyatta aingie akiwa wa tatu,” amesema Bw Kabogo.

Akitoa kauli yake kuhusu mikutano ya kisiasa ambayo imekuwa ikiendeshwa na viongozi wa kisiasa, Kabogo alisisitiza kuwa ndiyo imechangia kuongezeka kwa joto la kisiasa.

“Kwa nini watu wanaandaa mikutano ya kisiasa ambayo imegeuka kuwa kampeni, ilhali tumesalia na miaka miwili tushiriki uchaguzi mkuu? Inamaanisha kuwa tumeshinda ugonjwa wa Covid-19? La. Tuwache kampeni za mapema,” Kabogo amehimiza, akionekana kushangazwa na mikutano ya wanasiasa huku taifa likiwa limekodolewa macho na hatari ya virusi vya corona.

Kufuatia mikakati iliyowekwa na serikali kusaidia kuzuia kusambaa kwa corona, gavana huyo anasema ni ishara kuwa Rais Kenyatta pia ana uwezo kuzima mikutano ya kisiasa.

“Serikali imefanikisha kutekelezwa kwa kafyu ya kitaifa. Alivyofanikisha amri hiyo, Rais pia anaweza kutia kikomo kampeni za kisiasa zinazoendelea,” Kabogo akashauri.

Rais Kenyatta ameweka wazi kuwa azma yake ni kuafikia ahadi za maendeleo kwa Wakenya alizotoa 2013 na 2017 wakati akitetea kuhifadhi kiti chake. Amenukuliwa mara kadhaa akikashifu wanaofanya kampeni za kuchaguliwa 2022, akihoji ni mapema mno, na badala yake wanasiasa waliochaguliwa wajitume kufanyia wapiga kura kazi.

Tofauti kati ya Rais na Naibu wake, Dkt Ruto, zinaendelea kuonekana, hasa baada ya salamu za maridhiano Machi 2018, baina ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, maarufu kama Handisheki.

Mustakabali kati ya Rais Kenyatta na Bw Raila wanaoshikilia ni wa kuunganisha taifa, ulipelekea kuibuka kwa kundi la ‘Kieleweke’ linaloegemea viongozi hao na la ‘Tangatanga’ linaloegemea upande wa Naibu Rais Ruto.